SEHEMU ya kwanza ya ripoti hii jana, iliangazia mgonjwa wa TB sugu alivyonusurika kifo mara mbili na baada ya kupona kisha kuitunuku tuzo maalum Hospitali ya Rufani ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto (KIDH),iliyomtibu. Sehemu ya pili ya ripoti hii inabainisha ukubwa wa tatizo hili migodini. Endelea...
Samweli Rugemalila, ni mmoja wa wachimbaji wadogo Mirerani mwenye wafanyakazi 60 ambako baadhi ya wagonjwa wa TB sugu wanatajwa kutokea katika mgodi huo maarufu kwa uchimbaji wa Tanzanite.
Rugemalila anakiri katika eneo lake la mgodi kwa vipindi tofauti ikiwamo mwaka huu, wafanyakazi wake baada ya kupimwa walikutwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
"Kwa mwaka huu (2014) wafanyakazi wangu baada ya kupimwa afya zao katika mgodi wangu, ni mmoja tu ambaye alikutwa na TB na kuanza matibabu mara moja ili kutoruhusu maambukizi zaidi kwa wenzake.”
Hata hivyo, akilinganisha miaka zaidi ya miwili iliyopita, Rugemalila anasema kwa sasa hali ya ugonjwa huo katika migodi imeimarika.
Anasema wagonjwa si wengi kwa sababu mara kwa mara mashirika yanayojishughulisha na masuala ya tiba, huwafikia kutoa elimu na kupima wafanyakazi.
“Kesi nyingine ya wafanyakazi katika mgodi wangu kukutwa na TB ilikuwa ni zaidi ya miaka miwili na waligundulika wafanyakazi wawili tu. Mwaka huu mwezi wa pili walikuja wataalamu wa afya kutoka katika mashirika yanayojishughulisha na ugonjwa huu.
“Wafanyakazi walipewa elimu na baadaye kupimwa afya na ni mmoja tu mwenye jinsia ya kiume, mwenye umri wa miaka 55 alikutwa na TB na huyu alikuwa ametoka mgodi mwingine kuja hapa kwangu. Alianza matibabu yake na sasa yupo kazini,” anasema.
Rugemalila anasema huduma za matibabu zimesogezwa karibu. Mbali na Hospitali ya Kibong'oto, sasa Mirerani kuna zahanati ambayo wagonjwa wa TB wanapobainika migodini, kupatiwa dawa hapo.
“Mfanyakazi aliyeugua wewe kumwomba na kuongea naye ataona kama nimemwanika aliugua TB. Ninachoweza kukueleza TB migodini ipo, lakini kulinganisha na huko nyuma, hali kwa sasa ni nzuri kwa sababu matibabu yake yamesogezwa na elimu zinatolewa mara kwa mara.
“Kwa mwaka huu hadi mwezi Agosti katika mgodi wangu, mashirika yanayotoa elimu na kupima yameshakuja mara tatu, hii inasaidia sana.
“Wito wangu kama mmiliki wa mgodi kwa kushirikiana na serikali, tuendelee kuhamasisha vijana upimaji TB wa mara kwa mara kwa sababu dawa zipo na matibabu ni bure. Tusiposhirikiana kwa pamoja jambo hili halitakwisha na TB ni ugonjwa wa kuambukiza,” anasema.
Julai, 2023, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Makatibu Wakuu na Mameneja Mpango wa Programu za TB kutoka nchi 15 barani Afrika unaofanyika kwa jijini Arusha. Mkutano huu pamoja na mambo mengine ulijadili namna nchi za Afrika zinaweza kuja na ubunifu pamoja na mikakati mipya ya kutokomeza TB Afrika na duniani kwa ujumla ifikapo mwaka 2030.
Wakati kukiwa na mikakati hiyo, Hospitali ya Rufani ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto (KIDH), iliyoko Wilaya ya Siha, Kilimanjaro, kupitia Mkurugenzi wake, Dk. Leonard Subi, katika mahojiano maalum na Nipashe, anaweka wazi hali ilivyo hospitalini hapo.
“Kuhusu hali hospitalini hapa kwa wagonjwa wa TB sugu, wako wengi ambapo kwa mwaka hufikia wagonjwa hadi 400.
“Tukiangalia kiidadi inapungua. Waathirika ni makundi yote kuanzia umri wa miaka 20 hadi 59 lakini wanaume ni zaidi kutokana na shughuli zao na wengi wapo katika migodi,” anasema.
Katika mahojiano hayo yaliyofanyika Agosti 6, mwaka huu, Mkurugenzi huyo anafafanua kuwa wanaposema magonjwa ambukizi wanamaanisha magonjwa yote yenye umuhimu wa pekee katika jamii ya kuambukiza yanayosababishwa na virusi, bakteria, fangasi na protozoa.
“Sisi ndio wenye jukumu hilo tangu mwaka 2010 Hospitali ya Kibong’oto ilipotangazwa katika gazeti la serikali namba 828 la Novemba. Suala la TB kwetu ni moja ya ugonjwa kipaumbele ndio alama ya hospitali maana ndiko ilikoanzia. Lengo la sasa ndio hospitali pekee ya rufani ya ugonjwa wa TB sugu nchini.
“Bahati nzuri serikali inawagharamia wagonjwa wote wa TB ya kawaida na sugu katika matibabu na vipimo,” anasema.
Anasema wale wa TB sugu huwa wanawafuata nyumbani kokote waliko nchini endapo Mganga Mkuu wa Mkoa husika atasema huyo ni mgonjwa wa rufani.
“Si lazima kuja hapa Kibong’oto na hii ni kwa sababu tumeshatoa mafunzo na tumeshajenga uwezo na tunawapelekea dawa waliko kwa gharama za serikali.
“Tunawalipia vipimo vyao vya maendeleo vya kimatibabu huko waliko. Hospitali yetu inatoa huduma hizo za kibingwa.
“Na wengine tunakuta wana usugu wa dawa, yaani za mstari wa kwanza wamezimaliza, za mstari wa pili wamemaliza, tunapambana nao mpaka kuhakikisha wanapona,” anasema.
Dk. Subi anasisitiza kwamba serikali inawapatia huduma nzuri za kimatibabu, dawa pamoja na lishe ambapo hupatiwa chakula mara nne kwa siku.
“Wanapatiwa chakula bora ambacho hata nyumbani kwao yawezekana hawana. TB sugu inatibiwa kwa matibabu ya miezi tisa kwa hapa Tanzania. Japo tunataka kubadilisha kuwa miezi sita baadaye.
“Hapa hospitalini wagonjwa wa aina hii tunakaa nao takriban miezi sita. Wanalazwa pale wanapata huduma zote za kibingwa na ubingwa bobezi, lakini pia wagonjwa hao hao tunawapa tiba ya saikolojia.
“Kwa nini tiba ya kisaikolojia. Mtu anatoka nyumbani kwake anaishi nje zaidi ya miezi sita hivyo anahitaji tiba ya saikolojia ili wasikate tamaa. Katika tiba hii wengine huwa tunawapeleka mbuga za wanyama kule wanakwenda wanafurahi na kufurahisha akili na kuwaondolea msongo wa mawazo,” anasema.
Dk. Subi anaelezea tuzo maalum ambayo hospitali imeipokea kutoka kwa Labowa Ingwagwi, mkazi wa Babati mkoani Manyara, mmoja wa mgonjwa aliyewahi kutibiwa hospitalini hapo kuwa imeongeza motisha kwa watumishi wakiwamo waliokuwa wanamhudumia.
Anasema mwanamume huyo alifikishwa hospitalini hapo baada ya kupewa rufani na alipatiwa matibabu yaliyochukua muda mrefu hadi kupata nafuu.
Ofisa Muuguzi Hospitali ya Kibong’oto, Sarah Matoi, aliyehudumu hospitalini hapo tangu mwaka 1994 na kuwa miongoni waliomtibia Ingwagwi, anasema tuzo maalum waliyopokea kutoka kwa mgonjwa huyo wakati huo ni ya kipekee kwao na imewaongezea ari ya kufanya kazi kwa wito zaidi.
Anasema wagonjwa wengi hutoka maeneo ya mbali na wanapokaa muda mrefu hospitalini baadhi hadi miezi 18, hukumbuka nyumbani.
“Fikiria mtu unachomwa sindano miezi miwili mfululizo (siku 60), mgonjwa anavurugika akili, anapata msongo wa mawazo. Tunamshukuru Mungu wagonjwa wanapona vizuri na tunawapa ushauri ili tatizo lisijirudie,” anasema.
Matoi anasema wamekuwa makini kuhakikisha wahudumu wa afya hawapati maambukizi kwa kutumia vifaa vya kujifunika.
Pia, kuangalia mazingira upepo unakoelekea na kuhakikisha hewa inaingia na kutoka wodini na mara kwa mara kutoa elimu kwa wagonjwa wanapokohoa wazibe mdomo.
“Mgonjwa akitumia dawa ndani ya wiki mbili vimelea vinakuwa havina uwezo wa kuambukiza kwa haraka. Asilimia kubwa wagonjwa wetu wanatoka migodini hususan Mirerani.
“Kwa miaka ya nyuma 1998-2000 wagonjwa wa nje tuliokuwa tukipokea kwa siku walikuwa ni kuanzia 100, 2002-2024 kwa siku kliniki ya nje huwa karibu 60,” anasema Matoi.
Itaendelea kesho
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED