KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi amesema serikali imejipanga kutatua kero ya Stendi na Soko inayowakabili wananchi wa Lamadi mkoani Simiyu.
Dk. Nchimbi ameyasema hayo leo wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo hilo ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake itakayofanyika kwa siku saba katika Mkoa huo na Shinyanga.
Hata hivyo pamoja na majibu hayo kwa wananchi, alimpigia simu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa kutoa ufafanuzi wa kina kwa wananchi waliokuwa na shahuku ya kujua hatima ya changamoto hizo.
Akitolea ufafanuzi huo Mchengerwa amesema: "Rais amezingatia malalamiko hayo na alituelekeza kuhakikisha eneo hilo inapelekwa fedha ya ujenzi wa soko na ujenzi wa Barabara.
"Lakini pia kwa kuwa Kuna ukimya tutakuwa hapo (Lamadi) kuanzia mwezi ujao kuaona namna gani tutakwenda kufanya maboresho kwa sababu fedha tulionayo kwa sasa ni ya ujenzi wa soko la kisasa na barabara kwa kiwango Cha lami urefu wa kilomita nane" amesema Mchengerwa huku akishangiliwa na Wanalamadi
Ameongeza wataalamu watakao kwenda mategemeo yao ni kuona uwezekano wa kufanya tathmini na kuongeza ujenzi wa stendi na kwamba kuanzia mwezi ujao wanategemea kutangaza zabuni ya kuanza kwa ujenzi wa soko la kisasa na barabara.
Amewahakikishia wananchi wa Lamadi kwamba changamoto zao zitatatuliwa na suala la Stendi amelichukua na wanaangalia uwezekano wa kulijumuisha wakati wa ujenzi wa soko na barabara.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED