WAZIRI wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi ameagiza Idara ya Kilimo ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, kutumia vishikwambi kukusanya takwimu za wakulima wa michikichi wanaopatiwa miche ya kisasa ya zao hilo ili kuwa na taarifa sahihi za uzalishaji wa zao hilo.
Ametoa agizo hilo alipotembelea moja ya mashamba bora ya zao hilo ambalo limepandwa miche ya kisasa iliyozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) Kituo cha Kigoma.
Amesema miche hiyo imezalishwa kwa kutumia ruzuku ya serikali na hivyo ili kuwa na takwimu sahihi ni lazima maofisa kilimo watumie nyenzo walizopatiwa kukusanya taarifa na kuzihifadhi kwa ajili ya tathimini.
Amesema lengo la serikali kuhimiza uzalishaji wa zao hilo ni kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kupikia ndani ya nchi na kupunguza kiwango cha uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi ambacho kimekuwa kikigharimu fedha nyingi.
Prof.Kabudi anaendelea na ziara ya kikazi katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya ambako anakagua na kuzindua miradi ya maendeleo, kuweka mawe ya msingi na kufanya mikutano ya hadhara na wananchi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED