CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema kasoro tano zilizoonekana kwenye uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Wakazi, zinatoa doa uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 27,mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo (Oktoba 13,2024), Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, amesema wamefanya tahimini na kubaini kuna kasoro tano zinazopaswa kurekebishwa.
Amesema kasoro ya kwanza ni wasimamizi wa uchaguzi huo ambao ni Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kutotoa hamasa kwa wananchi inavyotakiwa kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwamo kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwenda kwa wananchi kupitia simu za mkononi ili kuwakumbusha.
“Licha ya kutengewa Bajeti ya Sh. bilioni 17.79 kwa ajili ya kuendesha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, TAMISEMI haijafanya jitihada zozote za maana kuhamasisha wananchi.
Kasoro nyingine ni wasimamizi wa vituo, takribani nchi nzima kukataa kutoa idadi ya wananchi waliojiandikisha katika siku husika, kwa mawakala hasa namba na jina la mwisho kuandikishwa pindi zoezi linapoahirishwa jioni ili siku inayofuata kujiridhisha kuwa hakuna majina yaliyoongezwa kinyemela.
“Hii ni dalili ya wazi kuwa wasimamizi hao wamekuwa wanaendelea kuandikisha kwenye daftari wapigakura wasiostahili kupiga kura, baada ya zoezi kufungwa katika siku husika,” amesema Ado.
Amesema jambo la tatu ni uandikishwaji wa watoto na watu wasio na sifa za kuandikishwa, baada ya chama hicho kupokea taarifa za watoto, hasa wanafunzi wasiotimiza umri wa kupigakura wakikusanywa kwenda kuandikishwa kwenye vituo.
“Mathalani, kwenye Halmashauri za Ubungo (mtaa wa Luguruni, Kata ya Kwembe),” alieleza Ado.
Pia amesema jambo la nne ni TAMISEMI kutoshusha maelekezo ya kuruhusu mawakala kuendelea kupokelewa vituoni siku yoyote ya uandikishwaji, kwa kuwa uandikishwaji unaendelea.
Ado amesema walibaini kuwa wa vituo bandia vya uandikishaji wapigakura, licha ya mwongozo wa uandikishaji kuweka bayana kuwa, kwa mamlaka za vijijini uandikishaji utafanyika kwenye vitongoji, baadhi ya wasimamizi wa vituo wameanzisha vituo zaidi bila kuwashirikisha wadau.
“Mathalani, Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Kilwa, ameongeza vituo vitatu vya Nyuni Kata ya Songosongo, Bwidi na Mbunju katika Kata ya Miguruwe.
Mathalani, kituo cha Nyuni, kipo katika Kisiwa kidogo cha wavuvi kisicho na makazi ya kudumu. Licha ya wadau kupinga na Msimamizi wa Uchaguzi kuahidi kusimamisha uandikishaji kwenye maeneo hayo, uandikishaji unaendelea,” amesema.
“Kuna mapungufu makubwa ambayo ni lazima Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), iyashughulikie ili kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unakuwa huru, wa haki na wa kuaminika.
“Bila uandikishaji wa haki, kwa hakika hakuna uchaguzi wa haki. Uandikishaji uliogubikwa na hujuma, udanganyifu na upendeleo huzaa uchaguzi mbovu na usio wa haki,”amesema
“Uchaguzi usio wa haki, mbali na kuwanyima wananchi haki yao ya kufanya maamuzi kwa kuwachagua viongozi wanaowataka, pia hutishia amani, usalama na ustawi wa Taifa,” amesema Ado.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED