Vijana 1,400 wamuenzi Nyerere kutembea Mwitongo hadi Mwanza

By Timothy Itembe , Nipashe Jumapili
Published at 07:44 AM Oct 13 2024
Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Picha: Mtandao
Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

IKIWA kesho ni kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, vijana 1,436 kutoka mikoa yote Tanzania, wameanza matembezi kwa ajili ya kumuenzi kutoka kijiji alichozaliwa cha Mwitongo, Butiama mkoani Mara, hadi Mwanza.

Maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 25 ya Mwalimu Nyerere ambayo yataambatana na kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, yatafanyika kesho jijini Mwanza na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluihu Hassan.

Matembezi hayo yamezinduliwa juzi na Makamu Mwenyekiti Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Rehema Sombi.

Sombi alisema matembezi hayo yanalenga kumuenzi Mwalimu Nyerere, Rais  Awamu ya Kwanza na kuwataka vijana, jamii kuendelea kudumisha amani iliyoasisiwa na kiongozi huyo.

Alisema matembezi hayo yatachukua siku tano hadi hitimisho ya kilele cha siku ya kuzima mbio  za Mwenge wa Uhuru, jijini Mwanza.

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa Mara, Mary Daniel, aliwasisitiza vijana kuunda vikundi na kuchangamkia fedha za mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ya asilimia 10 ya makusanyo ya ndani katika halmashauri, kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi.

Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, alisema safari hiyo ya matembezi ni ya kihistoria kutokana maandalizi ya Nyerere, alipoanzia mchakato wa kutafuta Uhuru wa nchi na kujikwamua kutoka mikono ya utumwa wa wakoloni na harakati zilizaa matunda.

Prof. Muhongo alisema vijana walioshiriki matembezi ya mshikamano kwenye taifa kuanzia Mwitongo, alipoanzia matembezi ya kwanza mwaka 1967  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenda Mwanza, wametia hamasa ya mfano wa kuigwa kwa wenye nia ya kufanya hivyo na ni moyo wa hali ya juu wa kizalendo.

Katibu Mkuu wa UVCCM, Jokete Mwegelo, alisisitiza kuwa matembezi hayo ni utekelezaji wa maazimio ya viongozi  yaliyoazimiwa  Agosti, mwaka huu, mkoani Iringa  kuwa yafanyike kwa lengo la kumuenzi Baba wa Taifa na yaanzie alikoanzia matembezi mwaka 1967 kijijini Butiama.