Ridhiwani ataka kutochagua watu kwa urafiki, fedha

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 08:53 AM Jul 21 2024
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete.
Picha: Mpigapicha Wetu
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete.

NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amewataka wananchi kushiriki katika uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa kwa kuangalia na kuweka mbele uzalendo badala ua kuchaguana kwa kujuana.

Ridhiwani ambaye ni Mbunge wa Chalinze, alisema hayo jana kwenye mkutano na wananchi wa Mkange wakati wa ziara yake katika jimbo hilo, mkoani Pwani.

Aliwasisitiza wananchi hao kushiriki katika hatua zote za uchaguzi kuanzia ngazi ya chini ya kujiandikisha kwenye daftari la mpigakura mpaka siku ya kupiga kura katika vituo.

"Hata kama kuna mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi ambaye yeye mwenyewe mnamwona wala hataki mambo hayo jamii pale inamtaja vizuri, mfuateni na mmwambie kama wewe mwenzetu kila tukikaa kijiweni tunasema kama kuna mtu mzuri wakutuongoza basi ni yule pale ambaye ni wewe utatuletea  mambo mazuri eneo letu. Basi  mfuateni na mwambie ili tukisaidie chama chetu.

"Lakini kutafuta wale marafiki zenu ambao mnauza nao mapori , kutafuta marafiki zenu mnaofanya nao ubadhirifu wa mali za umma, ni kukiingiza chama  kwenye mtihani mkubwa sana," alisema.

"Ninaamini viongozi ninyi ambao ni wanachama hamtafanya kosa hilo. Tuleteeni  watu ambao tukifika hapa watu wanaendelea na shughuli zao tukisubiri siku ya kupiga kura, tunapiga kura na maisha yanaendelea," alisisitiza.