Hii ndiyo maana halisi ya Pasaka

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 12:06 PM Mar 31 2024
Sehemu ya waumini wa dini ya Kikristo wakiwa katika ibada.
PICHA:MAKTABA
Sehemu ya waumini wa dini ya Kikristo wakiwa katika ibada.

PASAKA ni Sikukuu muhimu sana katika kalenda ya Kikristo na huadhimishwa na maelfu ya watu duaniani. Pamoja na umuhumi wake ukweli huo, watu wengi wanasherehekea Pasaka pasipo kuifahamu vizuri.

Sikukuu ya Pasaka, kiasili,  inapatikana katika Agano la Kale la Biblia Takatifu. Neno tunalolisikia mara kwa mara ‘Pasaka’ linatokana na neno la Kiebrania ‘pesach’ . Katika lugha ya Kiyunani ni ‘to pascha’, maana yake kuruka au kupita na katika Kiingereza neno ‘passover’, maana yake ni ‘pita juu’.

Kila familia ya Kiyahudi ilitakiwa kumchukua mwanakondoo wa kiume mwenye umri wa mwaka mmoja, asiye na kasoro na kumchinja jioni ya 14 ya mwezi wa Abibu/Nisani (Machi-Aprili). Sehemu ya damu ya mwanakondoo aliyechinjwa, ilinyunyizwa nje katika milango ya nyumba walizoishi. Malaika wakati wa usiku wa Pasaka, alipoona damu katika nyumba za Wayahudi (Waisraeli) alipita, hakuua wazaliwa wao wa kwanza. 

Kwa mantiki hiyo,  kwa damu ya mwana-kondoo aliyechinjwa, Wayahudi waliepuka hukumu ya kifo iliyokuwa juu ya wazaliwa wote wa kwanza wa Misri.  Hili lilikuwa pigo la mwisho la Mungu ambalo lisingewapa Wamisri fursa nyingine bali kuwaruhusu Waisraeli waondoke Misri ili kutimiza azma ya Mungu ya kukiokoa Kizazi cha Abrahamu, Isaka na Yakobo kutoka utumwani.  Kutokana na tendo hilo, Wayahudi walipata fundisho kuwa Mungu ni Mungu wa Wokovu.

Sikukuu ya Pasaka inaelezwa katika Kitabu cha Kutoka 12:1-14, 21-23; 34:25, 26 kwenye Biblia Takatifu. Waisraeli waliagizwa kula Pasaka wakati wa siku ya kuokolewa kutoka utumwani Misri. Pasaka hiyo iliadhimishwa katika kila jamaa, baba wa nyumba akiwa kiongozi - ni kama alifanya kazi ya ukuhani (Kut.12:21).

 Waisraeli waliendelea kuadhimisha Pasaka nyumbani mwao katika mwezi wa Abibu/Nisani kwa kutegemea mwandamo wa mwezi. Maadhimisho hayo yalichukua siku saba. Chakula  cha jioni maalumu na mkate usiotiwa chachu, divai, mimea  na kondoo hutolewa na familia nzima hukusanyika. Waisraeli waliadhimisha Pasaka hata Kabla ya Waamuzi na Wafalme. Waliadhimisha mahali palipoitwa Gilgali kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Yoshua 5:10-12. 

Baada ya miaka mingi kupita, utaratibu ulibadilika. Iliwapasa kufanyia Pasaka Yerusalemu, mahali pamoja pa kuabudia baada ya hekalu kujengwa. Walifanya hivyo kwa kufuata agizo la Mungu (Kumbukumbu la Torati 16:1-6). Hata sasa Wayahudi wanaadhimisha Pasaka, ingawa kuna mabadiliko machache. 

Kwa kuwa hakuna tena hekalu Yerusalemu ambako mwanakondoo anaweza kuchinjwa, sikukuu ya siku hizi ya Kiyahudi iitwayo ‘Seder’, haiadhimishwi tena kwa mwanakondoo aliyechinjwa. Chakula cha jioni maalumu na mikate isiyotiwa chachu, divai, na mimea hutolewa na familia nzima hukusanyika. Utaratibu wa maadhimisho huongozwa na kiongozi wa familia (baba). Wayahudi hawaadhimishi Pasaka kama tukio la kihistoria tu bali husherehekea uhuru wao pia, siku ya maisha mapya.

MAANA YA PASAKA KWA WAYAHUDI

Pasaka ilikuwa ya maana sana kwa Wayahudi. Kwa kifupi, Pasaka ilikuwa alama ya uhusiano kati ya Mungu na watu wake na pia alama ya agano. Mungu alisisitiza  kuwa yeye ni Mungu wa watu wake na atawaokoa toka utumwani. Pasaka pia ilikuwa alama ya watu wa Mungu. Wale waliokula Pasaka walikuwa watu wa Mungu, ndio  aliowachagua kuwa taifa lake takatifu.

Pia Pasaka ni alama ya utii. Kwa Wayahudi, itikio la kufanya Pasaka lilionyesha utii kamili wa agizo la Mungu. Pasaka pia ni kwa kuwa Wayahudi waliamini kuwa Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo alikuwa Mungu wa kweli.

Ni alama ya kuonyesha kuwapo kwa Mungu. Mungu alikuwa pamoja nao akipita na kuangalia mateso yao na kuwapitia asiwauwe wazaliwa wao wa kwanza. Waliamini kuwa Mungu yuko, anasema, anaagiza, anatuma watu wake na anasikia kilio chao.

Sambamba na hayo, ni alama ya hukumu kwa wasiomcha Mungu. Wamisri hawakuwa waamini wa Mungu bali walifuata miungu yao na uganga. Kwa  sababu hiyo  Mungu aliwapiga mapigo. Pasaka pia ni alama ya nguvu za Mungu. Miungu ya Wamisri haikupindua maagizo ya Mungu. Mungu alijidhihirisha kuwa Mungu mwenye nguvu. Hakuna kiumbe awaye yote anaweza kushindana naye.

Vile vile pasaka ni:- 

·         Alama ya mwisho wa mateso. Kabla ya siku ya Pasaka, Wayahudi walikuwa katika maisha ya shida na taabu nyingi kwa miaka mingi. Wengi walizaliwa katika mateso na kufia katika mateso Misri.

 

     i.        Alama ya wokovu. Kwa tendo la Pasaka, Wayahudi waliokolewa kutoka katika mateso na kifo hasa kwa wazaliwa wa kwanza. Kwa ajili ya kuokolewa ndiyo sababu Mungu aliwasisitizia sana kuwafundisha Watoto wao maana ya Pasaka (Kutoka 12:26,27). Alama hii ya wokovu haikuwa ya wakati huo tu, bali ililenga hata kwa wokovu wa wakati ujao.

 

    ii.        Alama ya mwanzo mpya wa maisha. Kwa teolojia ya Waisraeli Pasaka ilianzisha kitu kipya kabisa. Ni kwamba kila Myahudi alipata maisha mapya, maisha ya uhuru kamili. Wayahudi baada ya kutoka Misri waliendelea kusherehekea siku ya maisha mapya, siku ya uhuru. Katika siku ya uhuru Mungu alijitambulisha kwao kuwa ndiye Mungu wao na Musa atawaongoza. Farao hana tena madaraka juu ya taifa la Israeli.

  iii.        Ni alama ya kuungwa pamoja. Wayahudi (Waisraeli) waliokuwa wametawanyika kwa kufuata makabila yao 12 sasa waliunganishwa pamoja chini ya Mungu mmoja. Waisraeli walijitambua kwa uwazi zaidi kuwa ni taifa moja, lenye uongozi mmoja na kuabudu kumoja. Wote waliungwa kwa damu ya kondoo. Teolojia ya Agano la Kale inakaza sana kuhusu umuhimu wa damu hasa kama kiungo kati ya Mungu na watu na kati ya watu na  mtu.

   iv.        Alama ya shukrani kwa Mungu kwa tendo la wokovu na uhuru.

    v.        Alama ya kuwa na matumaini. Waisraeli mioyoni mwao walitoa kondoo wa Pasaka wakiwa na matumaini kuwa wazaliwa wao wa kwanza hawatauawa, hawatakaa Misri tena kwa kuwa ahadi ya Mungu itatimilika-agano alilolitoa kwa Abrahamu, Isaka, na Yakobo kuwa uzao wao utakuwa mwingi na watairithi nchi.

Pasaka ilikuwa ya msingi katika mafundisho ya imani ya Wayahudi katika nyakati za Agano la Kale na inaendelea kuwa msingi katika mafundisho ya imani ya Wayahudi na Wakristo katika nyakati za Agano Jipya. 

Katika Agano Jipya, inaelezwa kuwa akiwa na umri wa miaka 12, Yesu alipelekwa na wazazi wake Yerusalemu kula sikukuu ya Pasaka (Luka 2:41-50) na baadaye katika maisha yake, alikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kula sikukuu ya Pasaka (Yohana.2:13). Chakula cha jioni cha mwisho ambacho Yesu alikula na wanafunzi wake Yerusalemu, mapema kabla ya kusulubiwa msalabani kilikuwa ni Chakula cha Pasaka (Mathato 26:1-2, 17-29). Yesu mwenyewe alisulubiwa siku ya Pasaka ya Kiyahudi (Ijumaa) kama Mwanakondoo wa Pasaka.

PASAKA KWA WAKRISTO

Maadhimisho ya Pasaka kwa Wakristo ni utimilifu wa ahadi za Agano la Kale na za Yesu Kristo mwenyewe wakati wa maisha yake duniani. Ahadi hizo zinathibitishwa na tendo la kufufuka kwake. Ufufuko wa Yesu ni wa pekee kwani unapita kutoka hali ya kifo na kuingia katika maisha mengine, maisha ya umilele yasiyofungwa na mipaka ya wakati au mahali. Ni maisha yasiyokufa kamwe. 

Kama ilivyoelezwa awali, Wayahudi walikombolewa kwa damu ya mnyama (Mwanakondoo), bali Wakristo tumekombolewa kwa mateso na kifo cha Yesu msalabani ili wautoke katika utumwa wa dhambi na mwenendo usiofaa. Wokovu kwa njia ya damu ya Yesu Kristo, hupatikana kwa njia ya utii utokanao na imani (Warumi 1:5;16:26). Yesu Kristo ni pasaka kwa Wakristo, aliyetolewa kuwa sadaka (1Wakorinto 5:7) na ambaye anaishi kwa tendo la ufufuko. Yesu Kristo awaokoa katika nguvu za uovu na kuwaletea ukombozi kwa njia ya msamaha wa dhambi (Wakolosai 1:13).

Kufufuka kwa Yesu Kristo ni msingi wa imani ya Kikristo na kumeongeza thamani ya Ukristo na huduma ya Kanisa. Mtume Paulo anasisitiza akisema, “Kama Kristo naye hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni Bure” (1Wakorintho 15:14). Pia kufufuka kwa Yesu Kristo kumeleta tumaini jipya na uhai mpya wa kiroho kwa Wakristo.  Kufa na kufufuka kwa Yesu kumewaokoa na mauti ya kiroho (1Wakorintho Kor.10:16-17; 11:24-26) na kwamba, wafu watafufuliwa siku ya mwisho. 

Kufufuka kwa Yesu Kristo kumeleta furaha. Wakati wa Pasaka Wakristo wanakumbushwa kutokubeba habari mbaya zenye kuleta mateso, maumivu na kuondoa furaha. Watu wanapaswa kubeba habari zenye kuleta furaha. Kufufuka kwa Yesu kunawavuta Wakristo katika maisha ya kutokukata tamaa na kutokuishi maisha ya hofu. 

Sikukuu ya Pasaka inawakumbusha kuwa Mungu ana uweza.  Watu wakipatwa na huzuni, yeye ni furaha yetu. Wakipatwa na matatizo, yeye ni jibu na uponyaji.  Watu wasiangalie tu matatizo na changamoto wanazokutana nazo, bali waangalie ukuu wa Mungu katika maisha. Yeye ni msaada wetu wakati wa mateso. Jambo la msingi ni kuwa watii na kumtumaini.

Pasaka ni Sikukuu ya mabadiliko ya kiroho na si vyakula au mavazi tu. Haipaswi kusherehekewa kwa mazoea, bali watu waruhusu mabadiliko ndani mwao. Iwakumbushe watu kuacha mienendo na tabia mbaya kama vile ulevi, wizi, usaliti, ukatili, fitina, usaliti, uongo, mafarakano, uonevu, uvivu, uchoyo, ubinafsi, upendeleo na ulozi. Watu wanakumbushwa kujali na kuthamini watu wengine ikiwa shukrani kwa Mungu.