Ajali basi, Hiace yaua m/kiti UWT

By Halima Ikunji , Nipashe Jumapili
Published at 08:37 AM Jul 21 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao.
Picha: Maktaba
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao.

WATU wawili, akiwemo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Igunga, Zawadi William (60), wamefariki dunia huku wengine 12 wakijeruhiwa kutokana na ajali ya basi kubwa na ndogo.

Ajali hiyo ilihusisha basi la kampuni ya MUMUKI lililokuwa likitoka Mpanda kwenda Arusha kugongana uso kwa uso na gari dogo aina ya Toyota Hiace. 

Wakisimulia ajali hiyo iliyotokea katika kata ya Nanga, mashuhuda akiwamo Juma Iddy, walitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni dereva wa basi kuwa mwendokasi bila kuchukua tahadhari licha ya kwamba ni la mkusanyiko wa watu. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, alisema ajali hiyo ilitokea juzi majira ya saa 7: 00 mchana na kuwa ilisababishwa na dereva Richard Gabriel (42) aliyekuwa akiendesha basi lenye namba za usajili T 702 DJF aina ya HIGER. 

Alisema baada ya kufika Nanga wilayani Igunga, dereva huyo alifanya uzembe wa kutaka kuyapisha magari mengine matatu na kukutana uso kwa uso  na gari dogo aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili T 202 DHU. 

Kamanda Abwao alisema tayari dereva huyo anashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kutokuzingatia sheria za barabarani na kusababisha ajali na vifo.  

Akithibitisha kupokea miili ya marehemu na majeruhi hao 12, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Dk. Mirichades Magongo, alisema waliofariki dunia ni Zawadi Wiliam (60) na Kaseko Makami (40) wote wakazi wa wilayani hapa. 

Aliwataja majeruhi waliowapokea kuwa ni Theresia Masali (24), Kamwa Jilili (65), George Ndalu mkazi wa Dodoma, Batholomao John (26) mkazi wa Igogo, Mary Joseph  (37), Mary Sesu mtoto wa miaka miwili. 

Wengine ni Wilfred Kingu (28), Pendo Ngusa (58), Christopher Bizimana (35), Allen Joseph na Maria Ndelege (45) huku kati yao, wanne walipatiwa rufani kwenda Hospitali ya Misheni ya Nkinga kutokana na kuvunjika baadhi ya viungo.