Samia atoa kauli utekaji, mauaji watoto

By Paul Mabeja , Nipashe Jumapili
Published at 08:41 AM Jul 21 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema serikali isitupiwe lawama kutokana na vitendo vya utekaji na mauaji ya watoto vinavyoendelea hivi sasa nchini bali jamii inapaswa kuwajibika ili kukomesha hali hiyo.

Amesema jamii inapaswa kuwajibika ili kukomesha hali hiyo, huku akiwaomba machifu kuyakemea katika maeneo yao kwa sababu yanachafua taswira ya taifa.

Aliyasema hayo jana Ikulu ya Chamwino, jijini hapa wakati akizungumza na viongozi wa kimila pamoja na machifu kutoka mikoa yote nchini.

Rais alisema vitendo vya utekaji na mauaji ya Watoto, wakiwamo wenye ualbino, hivi sasa vimeibuka kwa wingi katika maeneo mengi nchini hali ambayo inapaswa kukemewa na kuchukuliwa hatua kali.

 “Hivi sasa vitendo vya utekaji pamoja na mauaji ya watoto vimekuwa vikiripotiwa kila siku na namna vinavyoripotiwa serikali ndiyo inalaumiwa sana wakati kule yanakotokea mambo haya viongozi wa mitaa wapo, lakini hata machifu wapo wamekaa kimya.

 “Nawaombeni mwende mkayakemee mambo haya, kwani yanatokea huko kwenye jamii zetu na yanachafua taswira ya taifa letu lenye sifa nje. Leo hii watu wakisikia mtu katekwa ama mtoto kuuwawa siyo picha nzuri.

“Mambo ya mauaji ya wenye ualbino yalishapotea kabisa, lakini sasa yanarudi kwa kasi na ukiuliza watu wanadai ni uchaguzi, lakini uongozi anatoa Mungu siyo kwa kuuwa mtu,” alisema Samia.

Rais Samia aliwataka machifu wote nchini kusimamia mila na desturi za nchi na kupinga vitendo ambavyo vinaharibu utamaduni wa mtanzania.

 “Maendeleo hayakwepeki lakini sasa lazima kama taifa tuzingatie mila na desturi zetu, tusifanye mambo ambayo ni kinyume na tamaduni zetu,” alionya.

Rais Samia aliagiza machifu kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba na sheria za nchi ili kuondokana na tabia ya kutoa adhabu ambazo zinavunja haki za binadamu na kudhalilisha utu wa mtu.

 “Lakini pia mkatatue migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikisababisha mauaji ya watu na kuleta uhasama miongoni mwa wanajamii na mara nyingi wakulima ndiyo wanaoonewa.

 “Mimi mwenyewe kuna kipindi nilikuwa ninalima mpunga kule Morogoro, kuna wakati mpunga ulistawi hadi nikasema umaskini sasa basi, lakini siku moja tu mfugaji aliingiza mifugo yake (shambani) ndani ya dakika kumi tu, hakuna kilichobaki na nilipompeleka polisi, anajibu kwa dharau tu, eti ‘ng’ombe kala majani siyo mpunga’ ”alisema.

Rais alimwagiza Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro, kuharakisha mchakato wa uandaaji wa mwongozo utakaotumika kuwatambua na kuwasimamia machifu kutekeleza majukumu yao.

 “Nikutake Waziri Ndumbaro huu mwongozo muuharakishe ili tupate kitu ambacho kitawatambua na kuwasimamia machifu, vinginevyo tukiacha kila mtu afanye anavyotaka tutarudi kule ambako kutakuwa na uvunjifu wa katiba,”alisema.

Katibu wa Umoja wa Machifu, Aron Mkomangwa, kwa niaba ya machifu aliishukuru serikali kwa kuwatambua na kuwashirikisha katika matukio mbalimbali ya kitaifa.

 Mkomangwa aliahidi kuwa wataendelea kushirikiana na serikali katika kulinda maadili na kuzingatia mila na desturi za Mtanzania.

 “Mheshimiwa Rais pamoja na mambo mengine,  bado tunakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo ukosefu wa jengo la ofisi ya makao makuu,”alisema.

Awali, Waziri Ndumbaro alisema wizara yake iko katika hatua za mwisho kukamilisha mwongozo ambao utasaidia kuwatambua machifu wote pamoja na kazi zao wanazofanya.

“Mwongozo huu ni utekelezaji wa maagizo yako mheshimiwa Rais ya kutaka kuwapo na utaratibu maalum ambao utakuwa unatumika kuwatambua machifu kuanzia ngazi za vijiji hadi mkoa,” alisema.