Kocha Kitambi aiweka Singida BS kimataifa

By Shufaa Lyimo , Nipashe Jumapili
Published at 09:34 AM Jul 21 2024
KOCHA msaidizi wa klabu ya Singida Black Stars, Denis Kitambi.
Picha: Mtandao
KOCHA msaidizi wa klabu ya Singida Black Stars, Denis Kitambi.

KOCHA msaidizi wa klabu ya Singida Black Stars, Denis Kitambi, amesema usajili walioufanya na uwepo wa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems anaamini timu hiyo itacheza michuano ya kimataifa msimu ujao.

Akizungumza na Nipashe hivi karibuni kutoka mkoani Arusha ambako timu hiyo imeweka kambi yake kujiandaa na msimu ujao, alisema malengo yao msimu ujao ni kuhakikisha timu hiyo inapata nafasi ya kucheza mashindano ya kimataifa.

"Kwa wachezaji waliopo ndani ya timu hii tuna matumaini makubwa ya kushiriki mashindano ya Kimataifa msimu ujao mashabiki wategemee burudani kutoka kwetu, uwepo wa wachezaji wenye uwezo na benchi zuri la ufundi itatufikisha pale tunapotaka kufika," alisema Kitambi. 

Aidha, alisema wachezaji wao wana viwango vya cha Kimataifa ambavyo vitaleta ushindani mkubwa msimu huo ambao unatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa. 

Alisema tangu ajiunge na timu hiyo wachezaji na viongozi  wamempa ushirikiano mkubwa hali inayompa matumaini ya kutimiza malengo yao. 

Kwa upande wake Ofisa Habari wa timu hiyo, Hussein Masanza akizungumzia hali ya kambi yao alisema kila kitu kinaenda vizuri huku morali yavwachezaji ikiwa juu. 

Amewahaidi mashabiki kupata furaha kutokana na aina ya wachezaji waliowasajili msimu huu.