Simba yakiri dili la mpanzu gumu

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 09:22 AM Jul 21 2024
 Elie Mpanzu.
Picha: Mtandao
Elie Mpanzu.

UONGOZI wa klabu ya Simba kwa mara ya kwanza umejitokeza hadharani na kukiri kuwa ilikuwa inamuwania kwa udi na uvumba winga wa AS Vita, Elie Mpanzu, lakini dili hilo limekuwa gumu ingawa bado inaendelea kupambana dakika hizi za mwisho za dirisha la usajili.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema jana kuwa tatizo si pesa, bali klabu yake haitaki kumuachia, huku pia ikiwa hata haisemi thamani halisi ya mchezaji huyo.

"Mpanzu dili lake limekuwa gumu, klabu yake imekuwa na changamoto sana, tatizo siyo pesa, ila inaonekana haipo tayari kumuachia, bahati mbaya ana mkataba nao na hata bei hawasemi, wangetuambia wanamuuza tungemnunua, kwa hiyo niwaambie wanachama na mashabiki wa Simba kwa sasa dili limekuwa gumu,  siwezi kusema atapatikana au lah lakini tunaendelea kupambana, lolote linaweza kutokea, hata hivyo kama ikishindikana basi tutaendelea na tulionao kwa sababu tuna kikosi bora," alisema Ahmed. 

Alisema hata hivyo bado wanaendelea kumfuatilia na ikishindikana dirisha hili hata dirisha lijalo watahakikisha wanakamilisha dili hilo.

Hii ni mara ya kwanza klabu hiyo kujitokeza hadharani kukiri kumuwania mchezaji huyo ambapo awali zilikuwa ni tetesi na hakukuwa na taarifa rasmi za kumuhitaji mchezaji huyo.

Wakati hayo yakiendelea, huko kambini nchini Misri, wachezaji wapya wa kigeni wa Simba wameonekana kulizungumzia zaidi tamasha la kila mwaka la klabu hiyo maarufu 'Simba Day'.

Mratibu wa klabu hiyo, Abbas Ally, akiwa Ismailia nchini Misri, amesema kwa sasa wachezaji wote wapya wa kigeni, wameonekana kuzungumzia tamasha hilo huku wengine wakiingiwa shauku kwani wanafahamu watakwenda kutambulishwa mbele ya umati wa mashabiki 60,000 huku baadhi yao ikiwa ni mara kwanza kuwashuhudia.

"Kiukweli kambini kila mchezaji mpya amekuwa na hamu sana ya kutaka kujua kuhusu Simba Day. Kama unavyofahamu ni tamasha kubwa sana kwa sasa Afrika, na imekuwa ni gumzo kubwa kwa hiyo kila mchezaji ana hamu ya kutaka kulishuhudia, pia wapo kwenye hofu kwa sababu wanaambiwa uwanja wa Benjamin Mkapa unaochukua mashabiki 60,000 unajaa wote, kwa hiyo katika mzungumzo ya kila siku hakuna sehemu ambayo wanakosa kuliongelea," alisema mratibu huyo.

Simba itakwenda kucheza mechi yake ya tamasha la Simba Day dhidi ya APR ya Rwanda, Agosti 3, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Tamasha hili mwaka huu litafanyika kwa mara ya 16 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009 na aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo kwa wakati huo, Mzee Hassan Dalali.