RIPOTI MAALUMU - 2 Wasaikolojia tiba waonya hatari ya kamari, uvutaji shisha kwa watoto

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 09:05 AM Jul 21 2024
Vifaa vinavyotumika kuvutia shisha.
Picha: Mtandao
Vifaa vinavyotumika kuvutia shisha.

HII ni sehemu ya pili ya ripoti hii inayoangazia kushamiri kwa kamari na uvutaji wa shisha katika makazi ya wananchi kunakohusisha watoto. Katika sehemu ya kwanza jana, kulikuwa na ushuhuda wa namna vitendo hivyo vilivyoenea Kinondoni mkoani Dar es Salaam, hususani eneo la Mwananyamala.

Katika sehemu hii ya pili, wasaikolojia tiba wanaeleza kwa undani athari za kiafya wanaocheza kamari na wanaovuta shisha, huku mamlaka za kiserikali zikianika hatua inazochukua kuthibiti vitendo hivyo. Sasa endelea...

Elizabert Mbuya, mfanyabiashara wa mgahawa ulioko eneo la Kabanakabana, Mwananyamala, anayechezesha pia kamari katika makazi ya watu, anakiri amekuwa akipokea watoto wa jirani wakitaka kucheza.

Mbuya anasema watoto hao wanapofika, huwafukuza na wakati mwingine kwa wale ambao wazazi wao anawafahamu huwajulisha.

“Hapa nina mgahawa kama unavyoona ninauza supu na chapati, lakini ninafanya biashara huko ndani ya kuuza bia na nina mashine hii ya kamari. Sijaweka tangazo la mtoto haruhusiwi.

“Ni kweli watoto huwa wanakuja hapa na fedha mfano Sh. 200 kutaka kucheza na hii ni kwa sababu biashara yangu iko katikati ya makazi ya watu ila huwa siwaruhusu,” anasema.

Siku  nne tangu kutolewe maagizo na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)  ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, kuhusu kero hizo zilizotolewa na wananchi, jana Nipashe ilishuhudia baadhi ya maeneo michezo hiyo imeondolewa, huku shisha ikidaiwa kuuzwa usiku mnene.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Sindano, Kata ya Makumbusho, Kinondoni,  Selemani Mohamed, akizungumza na mwandishi wa habari hii jana ofisini kwake, alisema wameanza kufanyia kazi maagizo ya Makalla aliyotoa Julai 17, mwaka huu.

Alisema tayari wenyeviti wa mitaa sita ya Kisiwani, Kichangani, Minazini, Mbuyuni na Makumbusho na wake, wameitwa na Mtendaji wa Kata na diwani na kukubaliana kukutana kesho (Jumatatu) kujadili hatua za kuchukua baada ya maagizo  kutolewa.

“Juzi (Julai 18) katika mtaa wangu tulikuta mashine za kamari kama 11, kati ya hizo, tano ziko kwenye vyumba na zingine nje ya nyumba kwenye makazi ya watu. Tunatoa  elimu hatutaki kuona watoto huko wakicheza kamari baadhi wamezificha,” alisema.

Mohamed alisema katika mtaa wake tatizo kubwa ni kamari ambazo baadhi ya wahusika walioko mtaani wamekutwa wana nyaraka za kufungua biashara hizo kutoka manispaa husika (Kinondoni), hivyo kupitia kikao kitakachofanyika kitaamua nini kifanyike.

“Unaponiambia mimi mtu wa chini nichukue hatua kidogo unanipa mtihani, ndio maana nimeshukuru tulivyosikia kesho kutwa (Jumatatu) kutakuwa na kikao ambacho kitajumuisha diwani, Mtendaji Kata na polisi kata naamini utatoka uamuzi utakaolingana na maelekezo yaliyotolewa awali,” alisema.

WATAALAMU WAONYA 

Msaikolojia Tiba kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Isaac Lema, anasema sheria imewekwa kwa ajili ya kumlinda mtoto chini ya umri wa miaka 18 ambaye mfumo wake wa akili unakua na haujakomaa.

“Mtoto anapojihusisha na michezo ya kamari au matumizi ya dawa za kulevya ikiwamo shisha, mfumo wake wa akili unatengeneza mazoea kwa urahisi zaidi na kuingia katika uraibu kuliko mtu mzima ambaye akili yake imekomaa anajua lipi ni sahihi na lipi si sahihi.

“Mtoto yupo kwenye kipindi cha kujaribu mambo na anapozoea anaweza kuingia katika tabia hatarishi kwa afya yake, mfano matumizi ya shisha ni hatari kwa afya na michezo ya kamari inaweza kumwingiza katika tabia za wizi ili kupata fedha za kucheza. Jamii inatakiwa kuwalinda watoto na vitu vyote ambayo ni hatarishi kwao,” anasema.

Kamishna wa Kinga na Tiba kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA), Dk. Peter Mfisi.

Kamishna wa Kinga na Tiba kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA), Dk. Peter Mfisi, anasema shisha ni tumbaku kama nyingine, lakini yenyewe huvutwa kwa kutumia bomba maalum.

“Shisha kama shisha ni dawa za kulevya ambazo haidhibitiwi na DCEA wanaodhibiti ni Wizara ya Afya. Lakini inapotokea mtumiaji amechanganya na dawa za kulevya kama bhangi au heroine hapo DCEA ndio tunahusika kwa sheria zetu.

 “Shisha yenyewe ina kiwango kikubwa cha tumbaku ambacho mtu anapovuta pafu moja ni sawa na aliyevuta sigara 100 na husababisha uraibu,” anasema. 

Akizungumza kama daktari, mtaalam Mfisi anasema ni vizuri serikali kutafuta uwezekano wa shisha kutouzwa kiholela.

Anashauri kutengwe maeneo maalum ya kuvutia katika hoteli na baa kubwa ambazo si rahisi mtoto kufika na wahusika wapewe leseni za muda kudhibiti na si kama sasa baadhi huduma hizo zinapatikana katika makazi ya watu.

“Uvutaji wowote wa sigara au shisha wewe unaweza ukawa unavuta unapotoa moshi nje watu wote waliokaribu na wewe wanapata athari sawa na anayevuta, Kama zinavutwa katika makazi au mtoto anavuta athari za kiafya ni kubwa zaidi,” anasema.

Meneja wa Leseni na Huduma za Sheria kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Catherine Lamwai.
Meneja wa Leseni na Huduma za Sheria kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Catherine Lamwai, anakanusha kwamba mashine zilizozagaa holela katika makazi ya watu ni zao.

Anafafanua kwamba Sheria ya Michezo ya Kubahatisha ya Mwaka 2003, kifungu 70 kimekataza watoto chini ya umri wa miaka 18 kucheza na kamari na kimetoa adhabu si chini ya milioni moja au kuzidi milioni tano au kifungo kisichozidi miezi 12 au adhabu zote kwa pamoja.

“Sheria inakataza mtoto kucheza kamari na hata kuonekana kwenye maeneo akizungukazunguka na pia inampa adhabu hata wewe unayemwona mtoto akizunguka ukamwacha,” anafafanua.

Catherine anasema katika sheria hiyo kifungu 82 (a) kinaruhusu GBT kuteketeza mashine zinazokamatwa ambazo zipo kwenye maeneo ambayo hayako kisheria au sheria haijaruhusu kuwapo au mtu kukutwa na mashine bila leseni.

Anasema huko nyuma walikuwa na kampeni ya kuelimisha wananchi kuzitambua mashine hizo ikiwa ni pamoja na zile ambazo hazina nembo zilizotapaa katika makazi ya watu ili wazikamate.

“Zile ambazo hazijafuata utaratibu wa kisheria hazitakiwi kuwapo, zinazotakiwa ni zilizofuata utaratibu wa kisheria. Ili mtu aruhusiwe kuleta mashine hizo nchini anapaswa kuwa na leseni ya michezo ya kubahatisha kwenye mchezo husika na inapoibiwa lazima aseme,” anafafanua.

Pia anasema leseni hutoka katika maeneo ambayo si karibu nyumba za kuabudu, hospitali na liwe rahisi kufikika na vyombo vya dola.

“Hazitakiwi kuwekwa katika duka la mangi (vyakula) ambako mtoto anaweza kutumwa. Lazima kuwekwe tangazo mtoto chini ya miaka 18 haruhusiwi. Tusiseme tu zimetapakaa. Je, umechukua wajibu gani kumlinda mtoto wako? umemwona mtoto wa jirani umemsaidiaje? ” anahoji.

Ofisa Habari Mwandamizi GBT, Zena Athuman, anasema baada ya kubaini kuzagaa kwa mashine hizo za kamari katika makazi walianzisha Kampeni ya Mlinde Mtoto iliyofanyika 2022/23.

“Tanzania tuna kampuni 53 lakini si yote yanayoendesha hizi mashine, kampuni moja inaweza ikawa na biashara zaidi ya moja. “Wanaosajiliwa wanatakiwa kukaa kwenye baa au maduka maalum ya kuchezea na kinyume na hapo hufanyika ukaguzi kuhakikisha sehemu kama inaruhusiwa kisheria.

“Kuna watu wameibuka ambao wanaendesha hii biashara bila kufuata utaratibu, hao ndio wanaoleta shida wamezisambaza mitaani katika makazi ya watu, mashine zinazoongelewa ni zile utazikuta kwa mangi, vibarazani au kwa mama lishe,” anasema.

Zena anasema mwaka 2023 walianzisha kampeni nyingine ijulikanayo kama ‘Fichua Tukomeshe Mashine Haramu’, inayoendelea hadi sasa kwa lengo la kuelimisha watu maeneo sahihi ya kufanya biashara hiyo kama sheria inavyoelekeza.

Anasema mashine walizosajili mpaka sasa ni 32,000 na tangu wameanza kampeni hizo watu 32 wamekutwa na hatia kisheria.

Kuhusu mapato yatokanayo na michezo ya kubahatisha, Zena anasema mwaka 2021/22 fedha iliyopatikana zilikuwa ni Sh. bilioni 144,  mwaka 2022/23 Sh. bilioni 170 na 2023/24 makadirio yao ni kupata Sh. bilioni 200.

Julai 17, mwaka huu, wakati serikali ikisema imekamilisha kanzidata ya wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya na kuanza uchunguzi.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi, alisema kila siku hospitalini hapo hupokea waraibu 900  wanaotumia dawa za usaidizi wa kuacha dawa za kulevya ‘methadone’.