DC, OCD matatani madai kuzuia amri ya mahakama

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 08:30 AM Jul 21 2024
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Deusdedit Katwale.
Picha: Maktaba
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Deusdedit Katwale.

Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Deusdedit Katwale na Kaimu Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), Seleman Mwampamba, wameingia matatani baada ya kudaiwa kuzuia utekelezaji wa amri ya mahakama.

Kutokana na madai hayo, viongozi hao ambao wanahusika pia na masuala ya ulinzi na usalama katika wilaya, wanatarajiwa kupandishwa kizimbani Agosti 28, mwaka huu, katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora.

Hatua hiyo inatokana na madai ya Juma Nombo (70) na Mohamed Nombo (68), wakazi wa Dar es salaam kwamba Katwale na Mwampamba wamezuia utekelezaji wa amri ya mahakama. 

Walisema juzi kwamba Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Tabora, lilitoa hukumu na amri kupitia shauri la maombi madogo Na. 15 la mwaka 2014 kati ya marehemu mama yao mzazi, Asha Shabani, ambaye alikuwa mwombaji  dhidi ya Kasawa Willa ambaye ni mjibu maombi.

Kwa mujibu wa wazee hao, Katwale anadaiwa ndiye aliyemwagiza OCD kutokutoa askari kwenda kusimamia utekelezaji wa amri iliyotolewa na mhimili huo wa serikali unaosimamia sheria na haki.

“Tunashangaa viongozi hawa ambao wamepewa dhamana ya kuongoza,kulinda  amani na kusimamia haki,wanajua sheria na kufahamu mipaka ya kazi zao pia wanatambua kuwa uamuzi wa mahakama huwa hauingiliwi. Tunasikitika sana kufanyiwa haya na kusumbuliwa,” walisema.

Juma ambaye ni msimamizi wa mirathi ya marehemu mama yao huyo aliyefariki dunia Julai 17, 2017 Mahakama hiyo  ilimpa ushindi Machi 21, 2024 na Mkasiwa Auction Mart ambaye ni dalali wa mahakama, alipewa amri ya kumwondoa Willa kupitia barua yenye kumb. Na.TBR/LHT/Misc. Land Appl.Na.15/2024. 

“Dalali alitoa notisi kwa Willa ya siku 14 kuondoa mali zake katika eneo letu lenye ekari 60 lililopo Kidatu Kata ya Mtendeni na OCD alipewa taarifa hiyo na kutakiwa kutoa askari wa kusimamia utekelezaji wa amri hiyo lakini alidai amepewa maagizo na DC kutotoa askari hadi atakapokutana na pande zote mbili zenye mgogoro,” alisema.

Alisema dalali huyo alitoa taarifa ya utekelezaji kazi kwa mahakama Mei 15, 2024 kupitia barua yenye kumb.Na.MAM,MAOMBI MADOGO Na.15/2014 akieleza yaliyotokea kwa OCD kuhusu agizo alilopewa na mkuu huyo wa wilaya.

Juma alisema Machi 23, 2024 alipigiwa simu na OCD kwamba wanahitajika kwa mkuu wa wilaya na walifika na kumuonyesha nyaraka zote lakini kiongozi huyo alidai atasikiliza pande zote mbili na kutoa uamuzi kitu ambacho hawakuafikiana naye.

Naye Mohamed alisema walikwenda kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, wakamweleza suala lao na kamanda huyo alimwagiza OCD kushughulikia   suala hilo kupitia barua ya Mei 20, 2024 yenye kumb.Na.GB.536/379/01/36.

 “Tuliwasiliana pia na (Mkuu wa Jeshi la Polisi) IGP Camilius Wambura kipindi akiwa Tabora na kumweleza shida yetu na aliahidi kulifanyia kazi na tulimwandikia Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, kumweleza kero yetu kupitia barua ya Mei 16, 2024 yenye kumb.Na.JK/TBR/3/2024 na nakala tukaituma Ikulu kwa Rais (Samia Suluhu Hassan),”alisema.

Alisema baada ya barua hiyo, mkuu huyo wa mkoa aliwakutanisha na mkuu wa wilaya na alimwuliza kinachoendelea kuhusu suala lao na kujibu kuwa analishughulikia lakini akadai alitoa kauli ya kejeli kwamba kama wameshindwa maisha warejee kwao Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa waraka uliotolewa na aliyekuwa Jaji Kiongozi Eliezer Feleshi kupitia barua ya Septemba 30, 2020 yenye kumb.Na. CHA.26/228/01/37, viongozi walielekezwa kuhusu vitendo vya kuingilia na kuzuia utekelezaji wa amri na tuzo za mahakama huku akihimiza uamuzi wa mhimili huo wa dola kuheshimiwa. 

Katwale alipotafutwa kutoa ufafanuzi kuhusu tuhuma hizo  na kwamba anakwepa kupokea wito wa kuitwa mahakamani hakupatika ofisini kwake kwa maelezo kuwa anaumwa. Hata alipopigiwa simu hakupokea na alipotumiwa ujumbe mfupi, awali alijibu yuko safarini na alipotumiwa ujumbe unaoeleza tuhuma hizo, hakujibu wala kutoa ushirikiano.

Kesi hiyo dhidi ya mkuu wa wilaya ya OCD yenye jalada namba 15946/2024 imepangwa kusikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora chini ya Jaji Mfawidhi, Adam Mambi.