Mndeme ataka makazi nishati safi mpango jinsia mabadiliko tabianchi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 09:51 AM Jul 21 2024
NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, anayeshughulikia Mazingira, Christina Mndeme.
Picha:Mtandao
NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, anayeshughulikia Mazingira, Christina Mndeme.

NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, anayeshughulikia Mazingira, Christina Mndeme, amewasisitiza wadau wa mazingira kuweka mkazo suala la nishati safi ya kupikia katika Rasimu ya Mpango Kazi wa Taifa wa Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi.

Amesema wanawake nchini hutumia muda mwingi kutafuta kuni kwa ajili ya kupikia badala ya kufanya shughuli za kujiingizia kipato. Kutokana na hali hiyo, alisema ni muhimu kupanga mipango ya kushirikisha nishati safi katika masuala ya kijinsia. 

 Mndeme alisema hayo juzi wakati akifungua Kikao kazi cha Wadau cha Kukusanya Maoni Kuhusu Rasimu ya Mpango Kazi wa Taifa wa Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi, jijini Dodoma.  

Alisema athari za mabadiliko ya tabianchi yameathiri sekta za kiuchumi ambazo wanawake, wanaume, watoto, wazee, vijana na makundi maalum hutegemea kwa maisha yao ya kila siku.  

Mndeme alisema sababu mbalimbali, zikiwamo majukumu yao kijinsia, utamaduni, umri, uchumi, mila na desturi huchangia makundi hayo ya jamii kuathirika na athari za mabadiliko ya tabianchi. 

“Hii ni hatua kubwa katika uwezeshaji wa masuala ya jinsia hapa nchini, kama mnavyofahamu. Tanzania ni mwanachama wa  Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris. Makubaliano ya Paris yanazitaka nchi wanachama kuandaa Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Programu ya Lima kuhusu masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya tabianchi,” alisema. 

Mkataba huo ulianzishwa mwaka 2014 katika mkutano wa 20 wa Nchi Wanachama wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP20) uliofanyika Lima, Peru. Madhumuni ya LWPG ni kuzihimiza nchi Wanachama wa Mkataba kuhuisha masuala ya jinsia katika mipango kazi ya kitaifa ili kutekeleza Mkataba na Makubaliano ya Paris.  

Katika utekelezaji wa mkataba huo,Ofisi ya Makamu wa Rais ni kiungo wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi nchini, inaratibu maandalizi ya Mpango Kazi husika.    

Mndeme alisema utafiti mbalimbali umeonyesha nchi zinazoendelea bado hazijahuisha Programu ya Lima katika mipango, sera na mikakati ili kuwezesha kuwa na takwimu za makundi hayo, usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake katika majadiliano ya kimataifa, uhuishaji wa masuala ya jinsia katika sera, mipango na mikakati ya Taifa na kujenga uwezo wa kifedha, utaalam, fedha na taasisi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.  

Serikali tayari imehuisha masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi katika Sera ya Taifa ya Mazingira (2021), Mpango Kabambe wa Mazingira (2022-2032), Mkakati wa Taifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (2021-2026) na Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2021-2026).  

Maandalizi ya Mpango Kazi wa Taifa wa Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi ni mwendelezo ya jitihada za serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabainchi kwa kwa makundi yote ya kijamii ili kuleta maendeleo endelevu nchini.