Utata Tril 1.7/- kutolewa BoT

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 08:59 AM Jul 21 2024
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT)  Emmanuel Tutuba.
Picha: Maktaba
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba.

SHILINGI trilioni 1.7 zilizotolewa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kutumiwa na serikali zimezua utata, mwandishi wa Nipashe Jumapili anaripoti.

Uchambuzi wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/23 uliofanywa na Taasisi ya WAJIBU umebaini utata huo.

Akiwasilisha ripoti za uwajibikaji 2022/23 zilizotokana na uchambuzi wa Ripoti za CAG uliofanywa na Taasisi ya WAJIBU, Meneja Programu za Utafiti na Miradi, Moses Kimaro, alisema jijini Dodoma mwanzoni mwa wiki kuwa katika mwaka huo wa fedha, serikali iliidhinishiwa na Bunge kukusanya na kutumia Sh. trilioni 41.48.

Hata hivyo, Kimaro alisema Taasisi ya WAJIBU imebaini kuwa ukaguzi wa CAG kuhusu Hesabu za Serikali Kuu kwa mwaka 2022/23, umebaini serikali ilikusanya Sh. trilioni 41.88, kukiwa na ziada ya Sh. bilioni 400.

Hata hivyo, makusanyo yaliyopelekwa Mfuko Mkuu ni Sh. trilioni 38.447. Sh. trilioni 3.433 hazikupita Mfuko Mkuu wa Serikali.

Uchambuzi umebaini kuwa serikali licha ya kukusanya trilioni 38.447 zilizopita Mfuko Mkuu, BoT iliipa (serikali) Sh. trilioni 40.18, hivyo Benki Kuu kuipa serikali Sh. trilioni 1.7 za ziada.

Vilevile, imebainika kuwa kati ya Sh. trilioni 3.433 ambazo hazikupita Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mwaka huo wa fedha, Sh. trilioni 3.197 zilipelekwa moja kwa moja kwenye miradi.
 
 Benny Mwaipaja, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Fedha, alipotafutwa na Nipashe Jumapili Jumanne ya juma hili kuzungumzia utata huo, aliahidi kutafuta majibu kutoka kwa wataalamu wa wizara.

Hata hivyo, tangu siku hiyo hadi tunaingia mtamboni, Mwaibaja hakutoa majibu kuhusu utata huo licha ya kukumbushwa Jumatano saa 8:12 mchana, Alhamisi 3:21 asubuhi na jana saa 7:49 mchana.

KUTOKA KWA CAG

Iliporejewa Ripoti ya CAG kwa Mwaka 2022/23 kuhusu suala hilo, inaonesha kuwa katika mwaka huo wa fedha, serikali ilikusanya Sh. trilioni 41.880 ikiwa ni zaidi ya bajeti ya Sh. trilioni 41.480 kwa Sh. bilioni 400.

Kulinganishwa na Sh. trilioni 38.298 zilizokusanywa mwaka 2021/22, CAG anaripoti kuwa alibaini ongezeko la asilimia tisa sawa na Sh. trilioni 3.582.

Tathmini ya CAG kuhusu mwenendo wa makusanyo katika kila chanzo kwa mwaka 2022/23 inaonesha makusanyo ya kodi Tanzania Bara yalikuwa Sh. trilioni 22.583 sawa na asilimia 95.5 ya lengo la kukusanya Sh. trilioni 23.652, hivyo serikali haikukusanya Sh. bilioni 1.069.

Kwa mwaka 2021/22, makusanyo hayo yalikuwa Sh. trilioni 20.945, hivyo kuwapo ongezeko la makusanyo kwa Sh. trilioni 1.638 sawa na asilimia nane.
 
 CAG anatipoti kuwa mapato yasiyotokana na kodi yaliyokusanywa na wizara, idara na sekretarieti za mikoa na taasisi nyinginezo yalikuwa Sh. trilioni 2.7095 sawa na asilimia 81 ya lengo la kukusanya Sh. trilioni 3.352, hivyo Sh. bilioni 643 hazikukusanywa. Kwa mwaka 2021/22, makusanyo ya eneo hilo yalikuwa Sh. trilioni 2.709 ya mwaka 2021/22, hivyo CAG amebaini ongezeko dogo.

Kwa upande wa makusanyo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, kwa mwaka 2022/23, CAG anasema walikusanya Sh. trilioni 1.222 ikiwa ni zaidi ya lengo la kukusanya Sh. trilioni 1.012 (asilimia 21) sawa na ongezeko la Sh. bilioni 21.

 Kulinganisha na makusanyo ya Serikali za Mitaa ya Sh. bilioni 892 ya mwaka 2021/22, CAG anasema alibaini ongezeko la Sh. bilioni 330 sawa na asilimia 37.

Upande wa misaada, katika mwaka wa fedha 2022/23, CAG amebaini misaada iliyopokewa ni Sh. bilioni 759 sawa na asilimia 69 ya lengo la kusaidiwa Sh. trilioni 1.101, hivyo kiasi cha Sh. bilioni 342 hakikukusanywa.
 Kulinganishwa na misaada ya Sh. trilioni 1.305 iliyopokewa mwaka 2021/22, CAG anasema amebaini kupungua kwa misaada kiasi cha Sh. bilioni 546 sawa na asilimia 42.

CAG anasema kuwa mikopo ya ndani, makusanyo yake yanayotokana na mikopo ankara za hazina, hati fungani na ufadhili wa ndani, kwa mwaka 2022/23 yalikuwa Sh. trilioni 6.124 ikiwa ni zaidi ya bajeti ya Sh. trilioni 5.780 sawa na ongezeko la Sh. bilioni 344 (asilimia sita).

Kulinganisha na mikopo ya Sh. trilioni 6.489 zilizokusanywa mwaka 2021/22, CAG amebaini kupungua kwa mikopo ya ndani ya Sh. bilioni 365 sawa  na asilimia sita.

Kwa upande wa mikopo ya nje yenye masharti nafuu, CAG anasema Sh. trilioni 5.523 zilipokewa katika mwaka wa fedha 2022/23 ikiwa ni zaidi ya lengo la kukopa Sh. trilioni 3.547 (Sh. trilioni 1.976 zikizidi sawa na ongezeko la asilimia 56).

Kulinganisha na mikopo ya Sh. trilioni 4.149 zilizopokewa mwaka 2021/22, hivyo CAG amebaini ongezeko la mikopo ya nje yenye masharti nafuu kwa Sh. trilioni 1.374 sawa na ongezeko la asilimia 33.

CAG pia anasema kwa upande wa mikopo ya nje isiyo ya masharti nafuu, Sh. trilioni 2.959 zilipokewa sawa na asilimia 97 ya lengo la kukopa Sh. trilioni 3.034, hivyo mikopo isiyo ya masharti nafuu ya Sh. bilioni 75 haikupokewa.

Mdhibiti anasema: "Mikopo isiyo na masharti nafuu imeongezeka kwa asilimia 64 au Sh. trilioni 1.150 kulinganishwa na Sh. trilioni 1.809 zilizopokewa mwaka 2021/22."

MATUMIZI
 CAG anafafanua kuwa kati ya Sh. trilioni 41.880 zilizokusanywa, Sh. trilioni 38.447 zilipokewa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali, hivyo kuwapo tofauti ya Sh. trilioni 3.4334.

Anasema tofauti hiyo inatokana na Sh. trilioni 3.656 zilizopelekwa moja kwa moja kwenye miradi kutoka kwa wadau wa maendeleo na makusanyo yaliyopelekwa Zanzibar ambayo hayapitii Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali pamoja na Sh. bilioni 223 zinazotokana na bakaa za makusanyo ya kodi za mwaka uliopita na  makusanyo mengine yaliyopokewa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali nje ya makisio ya bajeti.

 "Jumla ya matumizi yaliyofanywa katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ili kugharamia matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mwaka wa fedha 2022/23 yalikuwa Sh. trilioni 39.523 bila kujumuisha Sh. bilioni 665.80 zilizotolewa kama fedha zilizorejeshwa (refunds) na matumizi mengine kwenye jumla ya makusanyo ya Sh. trilioni 38.447, hivyo kusababisha nakisi katika Benki Kuu (BoT) ya Sh. trilioni 1.742 kufikia tarehe 30 Juni 2023," CAG anafafanua.