TFF: Twiga Stars watafanya vizuri WAFCON

By Shufaa Lyimo , Nipashe Jumapili
Published at 09:31 AM Jul 21 2024
Twiga Stars.
Picha: TFF
Twiga Stars.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema ubingwa walioupata timu ya taifa ya wanawake 'Twiga Stars' kwenye michuano ya Tunisia (Tunis Womens Cup 2024) utawasaidia kufanya vizuri kwenye fainali za Afrika za wanawake 'WAFCON' zitakazofanyika mwaka huu nchini Morocco.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mara baada ya kikosi cha timu hiyo kuwasili kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Rais wa TFF,  Wallace Karia aliipongeza timu hiyo kwa kufanya vizuri kwenye mashindano hayo na kupeperusha vema bendera ya Tanzania.

"Mashindano haya yalikuwa sehemu ya maandalizi kuelekea kwenye mashindano ya WAFCON ambayo yatafanyika mwaka huu kwani malengo yetu ni kuona timu inakwenda kushindana na si kushiriki," alisema Karia.

Aidha, alisema wameamua kuitumia michezo ya kirafiki ya kalenda ya FIFA ili benchi la ufundi la timu hiyo lihakikishe linaunda timu yenye ushindani kuelekea kwenye fainali hizoza Afrika.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Bakari Shime alisema amefurahishwa na viwango vilivyoonyeshwa na wachezaji wake katika mashindano hayo na kudai walikwenda kwa lengo la kutwaa kombe hilo.

Alisema kuelekea kwenye fainali za WAFCON, watakaa na kuzungumza na TFF kwa ajili ya kujadili mapungufu na changamoto zao kwa ajili ya kuhakikisha wanakwenda kufanya vema nchini Morocco. 

"Tumefurahishwa na mafanikio haya ambayo tumetumia kalenda ya FIFA kwa kucheza michezo mfululizo itakayotusaidia kufanya vizuri kwenye WAFCON," alisema Shime. 

Kwa upande wa wachezaji, nahodha wa timu hiyo, Anastazia Katunzi, alisema ushindi huo utawasaidia kuipeperusha vema bendera ya Tanzania na kuwataka watanzania waendelee kuwaamini kwa kuwa malengo yao ni kufika mbali. 

Timu hiyo ilicheza michezo miwili mchezo wa kwanza walicheza na Botswana na kutoka Suluhu ya kutokufungana wakati mchezo wa pili iliichapa wenyeji, Tunisia mabao 5-0 na kutwaa ubingwa huo.