Yanga yamalizana na Mzize 'kibabe'

By Saada Akida , Nipashe
Published at 06:44 AM Apr 19 2024
news
Picha: Yanga SC
Mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize.

WAKATI Azam FC ikiwasilisha ofa 'nono' la kutaka huduma ya mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wamemalizana na nyota wake kwa kumpa mkataba mpya, imefahamika.

Taarifa kutoka Yanga zinasema mshambuliaji huyo amesaini mkataba mpya wa miaka miwili na hivyo kumaliza ndoto za matajiri hao wa Chamazi kupata huduma yake kwa ajili ya msimu ujao.

Azam ambayo iliweka mezani ofa ya Sh. milioni 400 ili kumnunua Mzize ambaye anatajwa pia kutakiwa na timu moja ya England pia inataka kumsajili kiungo mshambuliaji wa Simba, Mzambia Clatous Chama.

Hata hivyo katika barua ya Azam, hakuna mahali ilikoandika katika maombi ya kumsajili Mzize, kutakuwa na makubaliano ya kubadilishana na mshambuliaji wake nyota, Prince Dube, ambaye kwa sasa yuko katika mgogoro na timu hiyo.

Akizungumza na Nipashe jana, Ofisa Habari Msaidizi wa Azam FC, Hashim Ibwe, alikiri wamepeleka ofa katika klabu hizo mbili (Yanga na Simba), kwa ajili ya kuhitaji kuwapata nyota wanne ambao watakiongezea nguvu kikosi chao.

Ibwe alisema mbali na kuweka dau kubwa kwa Mzize, pia wameahidi watamlipa mshahara kubwa endapo dili ya kumnasa mshambuliaji huyo litafanikiwa.

"Hatuishii kwa Yanga pekee pia tutaenda kwa Simba, wiki ijayo kuanzia Jumatatu tunapeleka ofa nyingine kwenye moja ya hizi klabu tukihitaji huduma ya moja ya mchezaji wao,” alisema Ibwe.

Ofisa huyo aliongeza mwaka huu wamedhamiria kufanya usajili 'mkubwa' kwa kuwanasa wachezaji 'muhimu' kutoka ndani ya klabu hizo mbili.

"Tumedhamiria na tuna mpango wa kusajili wachezaji wanne kutoka kwa Simba na Yanga, wachezaji hao ni pamoja na wazawa na wakigeni, tumejipanga kweli kweli," Ibwe alisema.

Aliongeza wameamua kufanya 'kweli' katika mchakato huo ili kuhakikisha msimu ujao wanakuwa na kikosi imara na kitakachowapa matokeo rafiki katika mashindano yote watakayoshiriki.

"Hatutaki masihara katika ofa hizo hakuna sehemu ambayo tunahitaji kubadilishana wachezaji bali, tumeweka ofa mezani," aliongeza Ibwe.