Mgunda: Kuna upungufu mkubwa wa kufanyia kazi

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 10:28 AM May 02 2024
Kaimu Kocha Mkuu wa klabu ya Simba, Juma Mgunda.
Picha: Simba SC
Kaimu Kocha Mkuu wa klabu ya Simba, Juma Mgunda.

KAIMU Kocha Mkuu wa klabu ya Simba, Juma Mgunda, amesema yapo mazuri aliyoyaona kwenye kikosi chake lakini kuna upungufu mkubwa unaotakiwa kufanyiwa kazi ili timu kuweza kupata matokeo mazuri kwenye mechi zilizobakia.

Akizungumza baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruagwa mkoani Lindi, Mgunda alisema ni lazima wafanyie kazi haraka upungufu waliouona ili kuepuka kupoteza pointi.

Alisema moja ya mambo aliyoyaona ni kutokuwapo kwa mawasiliano katika safu ya ulinzi ya timu hiyo pamoja na kupoteza nafasi nyingi za kufunga.

"Hii ndio mechi yangu ya kwanza tangu nimechukua timu, tumecheza vizuri na tuliishika mechi lakini baadhi ya makosa yametugharimu leo",

"Safu yangu ya ulinzi haikuwa na mawasiliano na hii ilipelekea hata kuruhusu goli la kusawazisha kwa wapinzani wetu, tunatengeneza nafasi lakini hatuzitumii, haya yote yanatakiwa kufanyiwa kwazi kwenye uwanja wa mazoezi ili mechi zilizobakia tuweze kufanya vizuri," alisema Mgunda.

Alisema baada ya mchezo huo wa juzi kwa sasa wanajiandaa na mchezo wao wa kesho dhidi ya Mtibwa Sugar.

"Matokeo ya mchezo huu yamepita kwa sasa kama nilivyosema tunarudi uwanja wa mazoezi kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Mtibwa, kama tutafanikiwa kupunguzu mapungufu yetu ni nina uhakika wa kufanya vizuri kwenye mchezo huu," alisema Mgunda.

Kwa matokeo hayo ya juzi, Simba imeendelea kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 47 baada ya kucheza michezo 22 ikizidiwa kwa pointi saba na Azam FC inayoshika nafasi ya pili baada ya kucheza michezo 24 sawa na vinara Yanga wenye pointi 62.