Amana kujipanga kupokea wagonjwa kwa njia ya TEHAMA

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 07:47 PM May 16 2024
Katibu Mkuu Wizara Afya kushoto Dk.John Kingu akitembelea miundo mbinu hospitalini hapo.
Picha: Pilly Kigome
Katibu Mkuu Wizara Afya kushoto Dk.John Kingu akitembelea miundo mbinu hospitalini hapo.

HOSPITALI ya Rufaa Mkoa wa Amana inajipanga kuanza kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa kupitia mfumo wa TEHAMA kabla hawajafika hospitalini hapo ili kuondoa msongamano na kurahisisha huduma zake.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk. John Kingu ameviambia vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo kuwa, katika kuboresha huduma katika hospitali za rufaa nchini serikali inatoa maagizo kwa hospitali hizo kuweza kuboresha huduma zaidi huduma kwa wananchi wake.

Amesema wagonjwa wanatakiwa watumie mifumo ya kuweka miahadi ya kupatiwa matibabu na kupangiwa siku na muda wa kumuona daktari husika na kupatiwa matibabu hivyo itasaidia na kurahisisha kuimarisha kutoa huduma kwa wagonjwa.

“Mtu kokote aliko awe anatoka Dar es Salaam ama mkoani basi atalazimika kupiga simu au kutumia mifumo ya barua pepe na mingine itakayowekwa kuomba kufika hospitalini hapa kutibiwa bila kujali simu ni ya kisasa au kitochi mfumo huo utawafikia” amefafanua

Wakati huohuo Dk. Kingu ameweza kuwakabidhi hati ya umiliki wa ardhi Hospitali hiyo wenye ukubwa wa hekari sita ambapo awali walikuwa wakiendesha shughuli za matibabu bila kuwa na hati miliki.

Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Amana Dk.Bryceson Kiwelu amesema kuwa agizo hilo la Katibu Mkuu wamelipokea kwa mikono miwili kwani walikuwa wanakabiliwa na changamoto wa msongamano wa wagonjwa na malamamiko mengi kutoka kwa wagonjwa kutokana na kila mmoja kutaka kutibiwa kwa wakati.

WhatsApp Image 2024-05-16 at 5.14.05 PM.jpeg 66.13 KB

Amesema wanajipanga kuanza kutoa elimu kwa wananchi na wagonjwa kuhusiana na matumizi ya teknolojia hiyo ya kutumia mifumo hiyo kabla ya kuanza kwa kutumia rasmi ili kuondoa sintofahamu kwa wagonjwa.

Amesema mfumo wa Tehama ulianza mwaka 2012 kwa kuwahudumia wagonjwa kwa kupatiwa majibu na huduma zingine lakini bila kutumia kwa kufanya miada kufika hapo ambapo wanajipanga kuanza muda si mrefu kutokana na gizo hilo.

“Mfumo huo utatusaidia kwa kiwango kikubwa kwani kinachotokea sasa hivi wagonjwa wote wanafika kwa wakati mmoja na kila mmoja ana ona yeye muhimu kupatiwa huduma kuliko mwingine” amesema Dk. Kiwelu.

Amesema wastani wa kupokea wagonjwa hospitalini hapo ni wagonjwa 650 hadi 700 kwa siku ambapo idadi hiyo imepungua toka kutokea kwa janga la Covid-19  ambapo awali walikuwa wakipokea wagonjwa 1000 na zaidi kuja kupata matibabu hospitalini hapo.

Aidha ziara hiyo iliweza kutembelea miradi ya hospitali hiyo ikiwemo kuona mtambo mpya wa kuchomea taka ambao utakuwa mradi wa kuingiza mapato ya ndani ambapo wataweza kupokea taka toka katika hospitali zingine na wataweza kuwahudumia huduma hiyo kwa kuwachomea kwa Shilingi elfu tano kwa kilo moja.