Hoja ya Lissu yaibua mvutano mahakamani

By Elisante John , Nipashe
Published at 10:56 AM Nov 12 2024
Wakili Tundu Antipas Lissu.
Picha:Mtandao
Wakili Tundu Antipas Lissu.

KESI ya Uchochezi inayomkabili Askofu Machumu Kadutu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la jijini Dar es Salaam, aliyeshitakiwa mkoani Singida, imechukua sura mpya, baada ya Wakili Tundu Antipas Lissu kuomba mahakama itupilie mbali shauri hilo, akidai mashtaka hayana mashiko.

Katika shauri hilo la jinai namba 19525 la mwaka 2024, Askofu Kadutu ameshtakiwa kwa kutamka maneno yanayodaiwa ya uchochezi wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa siasa.

Wakati wa mkutano huo wa siasa uliofanyika Juni 3 mwaka huu katika kijiji na kata ya Ibaga, wilayani Mkalama, mkoani Singida, ilidaiwa mahakamani na Wakili wa Serikali Almachius Bagenda kiongozi huyo wa kiroho alitenda kosa linaloweza kujenga chuki kwa wananchi dhidi ya askari na serikali yao kutokana na uchochezi.

Wakili Bagenda alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo kuwa, siku ya tukio, Askofu Kadutu alitamka maneno kuwa, "...naweza kukosea njia wakati wa kwenda lakini huwezi kukosea njia wakati wa kurudi, mmeshaifahamu njia.

"Walichofanya 2019 hakitajirudia... wangapi nyumbani mna majembe, wangapi mna visu nyumbani, wangapi nyumbani mna panga... ? Sasa mimi ninawaambia hivi kama kupitia polisi... kama wamerudia tena katika uchaguzi ili wapitishe wanavyotaka wao, haki ya Mungu safari hii haya majembe yatakuwa na matumizi mengine... wakiwa nanii na nyie mnafanyaje? Mnawananiii..."

Wakili Bagenda alidai maneno hayo aliyoyasema katika eneo la soko la zamani eneo la Madukani kwenye kijiji cha Ibaga, ni ya uchochezi na kinyume cha sheria.

Baada ya maelezo hayo, Wakili Lissu alimwomba Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida, Allu Nzowa kupitia shauri dogo alilolifungua mahakamani hapo, atupilie mbali shauri hilo, hoja iliyoibua mvutano wa kisheria, Wakili wa Serikali Bagenda akiipinga.

Hata hivyo, Hakimu Nzowa ilibidi aahirishe mahakama kwa muda wa nusu saa kutoa nafasi kwa pande zote kupitia vifungu vya sheria kabla ya kurejea tena kuendelea na mahakama.

Baada ya kurejea, upande wa serikali ilijibu hoja za Lissu, huku Lissu naye akiwa na hoja zake za kisheria. Hakimu Nzowa akaahirisha shauri hilo hadi Desemba 2 mwaka huu, atakapotoa uamuzi juu ya pingamizi lililowekwa na upande wa utetezi, unaodai shauri hilo halipaswi kuendelea kusikilizwa mahakamani.

Jopo la Mawakili wa Serikali liliongozwa na Bagenda, aliyesaidiwa na Nehemia Kilimhana na Michael Martin, huku Lissu akisaidiwa na Hemedi Kulungu.