Msuva atua kambini Stars, aongeza mzuka

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:29 AM Nov 13 2024
Winga wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva.
Picha:Mtandao
Winga wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva.

WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva, amewasili nchini na kuripoti kwenye kambi ya timu ya taifa 'Taifa Stars' kujiandaa na michezo miwili ya kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), dhidi ya Ethiopia na Guinea.

Msuva aliwasili nchini juzi akitokea nchini Iraq, ambako anacheza soka la kulipwa kwenye klabu ya Al Talaba na kuongeza 'mzuka' kwa timu hiyo kuelekea kwenye michezo hiyo.

Stars itaanza kuumana na Ethiopia nchini Congo Novemba 16 kabla ya kucheza nyumbani dhidi ya Guinea Novemba 19.

Winga huyo ni mmoja wa wachezaji waliorudishwa kwenye kikosi cha Stars baada ya kukosekana kwa muda mrefu kabla ya Kocha Mkuu, Hemed Suleiman 'Morocco', kuamua kumwita baada ya mashabiki wengi kutaka arudishwe.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), Clifford Ndimbo, amesema baada ya Msuva kuwasili wachezaji wengine wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, akiwamo nahodha Mbwana Samatta, walitarajiwa kuwasili jana.

"Msuva tayari amewasili na kuripoti kambini, kesho (leo) pia tunatarajia kupokea wachezaji wengine waliosalia, kwa maana hiyo kikosi chote cha wachezaji 25 walioitwa kitakuwa kimekamilika kufikia hapo kesho (leo) kwani wachezaji walioitwa wanaocheza soka la ndani wote wameshawasili," alisema Ndimbo.

Akizungumzia maandalizi alisema wanaendelea vizuri, ambapo asubuhi wanafanya mazoezi ya utimamu wa mwili na jioni wanafanya mazoezi kwenye uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.

"Kikosi kinaendelea na mazoezi kuelekea kwenye michezo yetu miwili ya kufuzu AFCON 2025, wachezaji wanafanya mazoezi mara mbili, wanaanza na utimamu wa mwili, na jioni wanafanya mazoezi kwenye Uwanja wa KMC, mkakati ni kuishinda michezo yote miwili kwa sababu tukifanya hivyo hatutoangalia mechi ya mtu yoyote, ila tukidondosha, ndipo tutaanza kutazama wengine na kuombeana mabaya, hatutaki hilo litokea," alisema.

Stars inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi H, ambapo imejikusanyia pointi nne, DR Congo ikiongoza kwa pointi 12 na Guinea ikiwa nafasi ya pili ikiwa na pointi sita.

Timu mbili kwenye kundi zinafuzu kucheza fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.