NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuepuka makundi ili kupata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu, 2025.
Alisema hayo jana jijini hapa alipokuwa akizungumza na wana CCM, kwenye Mkutano Mkuu wa CCM, Jimbo la Dodoma mjini.
Alisema kama CCM inahitaji ushindi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025, wanachama wanapaswa kuvunja makundi yao na kuwa kitu kimoja kukipigania chama.
“Kama tunahitaji kushinda ni lazima kuwa kitu kimoja kufanya kazi kwa ushirikiano tutofautiane katika vikao vyetu vya ndani, lakini tukitoka nje tuwe kitu kimoja kwa ajili kukipigania chama chetu kushinda kwenye chaguzi hizo,” alisema Dk. Biteko.
Aidha, alisema ana imani kuwa CCM itafanya vizuri kwenye chaguzi zote hizo kutokana na maandalizi yanayoendelea kufanyika ndani ya chama.
“Sioni kama kuna chama kingine ambacho kimejiandaa kama ilivyo kwa CCM, lakini pia licha ya maandalizi hayo pia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi uliofanywa na chama chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, vinatosha kabisa kukipa ushindi wa kishindo chama chetu,” alisema.
Kuhusu changamoto zilizopo kwenye Jimbo la Dodoma mjini, ikiwamo kukithiri kwa migogoro ya ardhi Dk. Biteko aliziagiza mamlaka zinazo husika kuipatia majibu ili wananchi wapate haki yao.
“Kuhusu migogoro ya ardhi katika jiji la Dodoma kama ilivyo elezwa awali na Mbunge Mavunde, niwaombe viongozi wa serikali hasa wale waliopo katika wizara husika kupatia ufumbuzi ili wananchi wapate haki yao na kwa wakati,” alisema.
Vilevile, kuhusu uhaba wa maji katika Jiji la Dodoma Dk. Biteko alisema Wizara ya Maji inapaswa kutekeleza maagizo ya Rais ya kuchimba visima virefu ili wananchi wapate huduma ya maji ya uhakika wakati wakisubiri miradi mikubwa ikamilike.
“Wakati tunasubiri miradi mikubwa ya bwawa la Farkwa pamoja na kutoa maji katika Ziwa Victoria, tunapaswa kuendelea kuchimba visima virefu ili kukabilina na tatizo la uhaba wa maji katika jiji la Dodoma,” alisema.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi katika jimbo la Dodoma kwa kipindi cha miaka minne Mbunge wa Antony Mavunde, alisema pamoja na mafanikio yaliyopatika, bado zipo changamoto kadhaa.
“Kutokana na serikali kuhamia Dodoma mahitaji ya maji yameongezeka na kusababisha mgao wa maji kwani hivi sasa mahitaji ya maji ni lita milioni 147 kwa siku na uzalishaji ni lita milioni 97 hivyo kufanya upungufu kuwa ni lita milioni 68 kwa siku,” alisema Mavunde.
Pia, alisema katika kipindi cha miaka minne wamepokea fedha Sh. trilioni 1.5 kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo la Dodoma Mjini.
Alisema fedha hizo zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwamo ujenzi wa uwanja wa ndege Msalato, barabarani ya mzunguko kilomita 112.3, ujenzi wa uwanja wa maonyesho ya NaneNane ya kudumu na mji wa serikali Mtumba.
Alitaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu, chuo cha ufundi, soko la kisasa la Machinga, hospitali, vituo vya afya na zahanati, shule za sekondari na msingi na miradi ya maji.
Katibu wa CCM, Mkoa wa Dodoma, Pili Mbanga, alisema wanaendelea na maandalizi mbalimbali ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika uchaguzi wa serikali za mitaa, mwaka huu.
Alisema jumla ya wanachama 17,657 wameteuliwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika Novemba 27,2024.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED