KAMPUNI ya The Guardian Ltd inayochapisha magazeti ya Nipashe na The Guardian, kwa kushirikiana na Tanzania Media Foundation (TMF), imezindua dawati la uandishi wa habari wa tija kwa lengo la kuboresha maudhui yake.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa dawati hilo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya The Guardian Ltd, Jackson Paulo, alisema anaamini mradi huo utakuwa na matokeo mazuri.
Alisema mradi huo utaanza Novemba 18 mwaka huu na utafanyika kwa kipindi cha mwaka mmoja.
"Ni mradi ambao ukiuangalia unaona kabisa umezingatia weledi na ambao unaona mwisho wa siku utaleta matokeo mazuri siyo tu kwa waandishi wa habari, bali pia kwa kampuni na umma.
"Kwa hiyo, sisi (The Guardian Ltd) tumeupokea, tutasapoti kwa mikono miwili na tunategemea tutaongeza ile asilimia ya uandishi wa habari wa tija kwa kiwango cha kutosha. Matamanio yangu ni angalau kwa mwaka wa kwanza, uandishi wa habari wa tija utaongezeka na tutakuwa na habari nyingi za aina hiyo (za maslahi ya umma)," alisema.
Kiongozi huyo wa The Guardian Ltd, alisema mradi huo unakwenda sambamba na kaulimbiu ya kampuni hiyo ya kuamini kwenye kitu kizuri ambacho hakipatikani mahali pengine isipokuwa katika kampuni hiyo.
"Falsafa yetu hapa ndani tunaamini katika ‘high value content’ (maudhui yenye thamani kubwa), ambayo haiko kila mahali... Kwa hiyo, lengo lenu (TMF) linaendana na sera yetu, hivyo tumekutana," alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa TMF, Danstan Kamanzi, alisema dawati hilo litahusisha waandishi wa habari, wahariri wabobevu, wataalamu wa sekta (eneo) husika na wanasheria, hivyo waandishi wataandaa na kuchapisha habari zinazohusu masuala mahsusi ikiwamo elimu, afya, kilimo, mazingira, siasa na mengineyo, yaliyofanyiwa uchunguzi wa kina ili kuleta matokeo chanya kwa jamii.
Kamanzi alisema TMF inaamini katika kuwajengea uwezo waandishi wa habari na kwamba wakati wote wamekuwa wanasisitiza uandishi wa habari wa tija ambao ndio wenye manufaa kwa umma.
Ni uandishi ambao Kamanzi alisema unafanyika kwa kiwango cha chini nchini. Akirejea utafiti wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wa mwaka 2022, Kamanzi alisema maudhui ya vyombo vya habari nchini yanaonesha uandishi wa aina hiyo unafanyika kwa asilimia nne tu nchini.
Alisema uandishi unaofanywa kwenye vyombo vya habari nchini, haujafikia viwango vizuri kwenye eneo hilo la uandishi wa habari wa tija (habari zinazojikita katika kumulika uwajibikaji na maslahi ya umma).
Kamanzi alisema utafiti huo wa SJMC unaonesha ubora wa maudhui ya vyombo vya habari nchini kwa mwaka 2018 ulikuwa ni asilimia 27, mwaka 2021 ulikuwa asilimia 22 na mwaka 2022 ulikuwa wa asilimia 30.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED