KIKOSI cha Yanga kimeanza rasmi mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan, utakaochezwa, Oktoba 26 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kikiwa chini ya Kocha Mkuu Miguel Gamondi ambaye ilitajwa kuwa angepewa mkono wa kwaheri.
Kikosi hicho juzi kilianza mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam, chini ya kocha huyo na kuvunja tetesi kuwa 'ndoa' ya kocha huyo na Yanga imevunjika na kuendelea na maandalizi bila wasiwasi wowote.
Gamondi alionekana kwa mara ya kwanza juzi baada ya mchezo dhidi ya Tabora United, Alhamisi iliyopita uliochezwa, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi wenyeji wakipoteza kwa mabao 3-1.
Baada ya mchezo huo, kukawa na tetesi nyingi zilizomhusu kocha huyo raia wa Argentina kuwekwa kikao na mabosi wake, kueleza ni kwa nini kikosi kimepoteza michezo miwili mfululizo na kuonekana kushuka uwezo, huku pia kukiwa na taarifa za kutoelewana na baadhi ya wachezaji.
Pamoja na taarifa hizo, habari za ndani zinasema kulikuwa na mpango wa kumtimua, ingawa zilikanushwa baadaye.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Klabu hiyo, Alex Ngai, aliibuka na kusema tetesi za kwamba klabu hiyo kumtimua Gamondi na kumleta kocha mwingine hazina ukweli wowote na kuwataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kutokuwa na wasiwasi wowote kwani viongozi wa Yanga bado wana ushirikiano na benchi la ufundi.
"Yanazungumzwa mengi, lakini niwahakikishie wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa viongozi wote wa Yanga wapo vizuri, tuna ushirikiano na benchi la ufundi, tutakaa na kufanya tathmini na tunaendelea na maandalizi ya mechi yetu dhidi ya Al Hilal ya Sudan, " alisema Ngai.
Hata hivyo zipo taarifa zinasema kuwa mpango huo ulikuwapo, lakini viongozi waligawanyika huku baadhi wakihofia presha ya mashabiki baada ya tukio hilo pamoja na kuwa ni muda mfupi uliobaki kuelekea kwenye mchezo wa kimataifa dhidi ya Al Hilal.
Zipo pia taarifa zinazosema kuwa mpango huo upo pale pale, lakini utafanyika kwa wakati unaofaa lakini si sasa huku ikidaiwa kocha raia wa Algeria, Kheireddine Madoui ndiye anayeandaliwa kuchukua nafasi yake.
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ally Kamwe, amesema wameanza rasmi maandalizi ya Ligi ya Mabingwa wakiwa chini ya Gamondi na kuzima maneno yote kuwa anaondoka.
"Taarifa yetu imenyooka na haina konakona, kocha yupo sana Jangwani, mengine yatabaki ni uamuzi wa viongozi, wakiona muda wake bado atabaki, wakiona inatosha basi, lakini niseme bado kocha yupo na amekiongoza kikosi kwenye maandalizi kuelekea mchezo wetu wa kimataifa dhidi ya Al Hilal Omdurman, hatuwezi kujibu taarifa zote za mitandaoni lakini ukweli umeonekana," alisema Kamwe.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED