Mabao 164 yafungwa Ligi Kuu mpaka sasa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:18 AM Nov 13 2024
Mabao 164 yafungwa Ligi Kuu mpaka sasa.
Picha: Mtandao
Mabao 164 yafungwa Ligi Kuu mpaka sasa.

JUMLA ya mabao 164, yamefungwa kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara hadi kufikia raundi ya 10 na baadhi ya mechi za raundi ya 11.

Idadi hii ya mabao ni chache ikilinganishwa na jumla ya mabao 184, yaliyofungwa kwenye michezo ya raundi 10 tu ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita.

Kwa mujibu wa takwimu za dawati la michezo la Nipashe, mabao hayo yamefungwa na wachezaji 98, katika michezo 83 ambayo imechezwa mpaka sasa ambapo ligi hiyo imesimama kupisha kalenda ya FIFA ambapo wachezaji wamekwenda kuunda kikosi cha timu zao za taifa kwa ajili ya kutafuta tiketi ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), zinazotarajiwa kucheza mwakani nchini Morocco.

Kati ya mabao hayo, 19 ni ya mikwaju ya penalti, na mawili ni ya wachezaji kujifunga wenyewe.

Wachezaji waliojifunga wenyewe ni Fred Tangalo wa KMC, aliyejifunga katika mchezo ambao timu yake ilicheza dhidi ya Azam FC,  Septemba 19, mwaka huu, Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, ikipokea kipigo cha mabao 4-0 na Kelvin Kijili wa Simba akijifunga Oktoba 19, mwaka huu ilipocheza dhidi ya Yanga, na lilikuwa bao pekee kwenye mchezo huo, Simba ikifungwa bao 1-0.

Katika michezo 83 iliyochezwa mpaka sasa, takwimu zinaonyesha kuwa 62 imetoa washindi na mechi 21 ziliisha kwa sare.

Takwimu zinaonyesha kuwa katika michezo 62 ambayo imetoa washindi, mechi 38 timu zimepata ushindi zikiwa nyumbani na michezo 24 imetoa washindi kwa timu zilizocheza zikiwa ugenini.

Jumla ya penalti 25 zimetolewa hadi kufikia sasa, huku 19 zikitinga wavuni na sita zikiota mbawa.

Wachezaji Jean Charles Ahoua wa Simba na Ogochukwu Morice wa Tabora United wanaongoza kwa kufunga mabao mawili ya penalti kila mmoja.

Ahoua, alifunga penalti zake mbili, Simba ikicheza dhidi ya Dodoma Jiji na kushinda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma, Septemba 29 mwaka huu, na dhidi ya KMC Jumatano iliyopita, Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam akiiongoza timu yake kushinda mabao 4-0.

Ogochukwu, alifunga penalti yake timu yake ilipocheza dhidi ya Pamba Jiji na kushinda bao 1-0 na Mashujaa FC, ikishinda pia bao 1-0.

Wachezaji wengine waliofunga penalti moja moja ni Djuma Shaaban wa Namungo, Heritier Makambo na Shedrack Asiegbu wote wa Tabora United, Salum Kihimbwa wa Fountain Gate, Hassan Dilunga wa JKT Tanzania, Nurdin Chona na Jumanne El Fadhil wa Prisons, Stephane Aziz Ki wa Yanga, Leonel Ateba wa Simba, Marouf Tchakei wa Singida Black Stars, Ismail Mgunda wa Mashujaa FC, Feisal Salum wa Azam FC, Ibrahim Elias wa KMC na Lulihosh Heritier wa Dodoma Jiji.