MBUNGE wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara, ameibua madai bungeni kuhusu ukusanyaji kodi kusababisha madhara eneo la Sirari, ikiwamo kijana mwenye bidhaa za plastiki kufariki dunia kutokana na kusukumwa kwenye mtaro na gari lililokuwa linatumiwa na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Akiomba mwongozo kwa kiti kwa kutumia Kanuni ya 76 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Waitara amesema wakati anapata majibu ya serikali kwenye swali la nyongeza la swali lake la msingi la 344 alieleza utaratibu unaotumika kukusanya kodi kwenye eneo hilo umesababisha madhara hayo.
Amesema gari hilo lilikuwa likimkimbiza kijana huyo na kumsukuma kwenye mtaro na kufariki dunia, tunashuhudia wengine wakipigwa hadi risasi.
“Nilidhani ingependeza sana kauli ya serikali, je, ni sahihi kutafuta kodi ya serikali kwa njia ya damu? Yaani unakusanya kodi kwa kuua watu na sio mara moja watu wetu wa TRA kule Sirari wana mipini ya jembe wanapiga vijana wa Tarime nadhani serikali itoe kauli juu ya hili ili wachukue kodi kistaarabu na kama kuna mtu ana magendo achukuliwe hatua bila kujenga chuki kwa watu wetu dhidi ya vyombo yetu vya ulinzi na usalama na TRA,” amesema.
Akijibu mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Deodatus Mwanyika amesema; “Mheshimiwa Waitara hapa kiti hakina nyaraka yoyote ya kuhakiki hilo jambo unalosema kwa hiyo nalipokea na tutarudi kwenu au kwako kadri kanuni zinavyoturuhusu.”
Hata hivyo, amemshauri Mbunge kupeleka swali la msingi ili kupata majibu ya serikali.
Awali, katika swali lake la msingi, Mbunge huyo alihoji lini serikali itaweka kituo kidogo cha forodha katika Kata ya Itiryo/Bikonge pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa kupata bidhaa kutoka Kenya.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba amesema kituo cha forodha Kata ya Itiryo/Bikonge ni miongoni mwa vituo tarajiwa vya forodha vitakavyofanyiwa tathmini na Mamlaka ya Mapato Tanzania katika mwaka 2024/25.
“Tathmini itafanyika kwa kuzingatia vigezo mahsusi ikiwamo uwiano wa gharama za ukusanyaji wa mapato na kiwango cha kodi kinachotarajiwa kukusanywa katika kituo hicho. Endapo kituo hicho kitakidhi vigezo, mchakato wa uanzishaji wake utaanza kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema.
Amewaelekeza wafanyabiashara wanaotumia mpaka wa Tanzania na Kenya uliopo Kata ya Itiryo/Bikonge, kuendelea kutumia vituo rasmi vya forodha vya karibu ikiwamo Kituo cha Forodha cha Sirari ili kurahisisha zoezi la ulipaji kodi na ukusanyaji wa mapato ya serikali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED