Gamondi aichambua Mamelodi kwa Yanga

By Saada Akida , Nipashe
Published at 01:09 PM Mar 20 2024
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.
#PICHA: YANGA SC
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.

HUKU wengi wakiipa nafasi zaidi Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwenye mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga Machi 30, mwaka huu, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ameichambua timu hiyo na kusema hakuna lisilowezekana kwa kuwa watakuwa 11 kwa 11 uwanjani na si vinginevyo.

Yanga itaikaribisha Mamelodi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na baada ya hapo timu hizo zitarudiana Aprili 5, mwaka huu, nchini Afrika Kusini na mshindi wa jumla atatinga nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Akiwachambua wapinzani wao hao jana, Gamondi amesema ubora wa kikosi na bajeti ya usajili wa Mamelodi Sundowns tofauti na Yang, lakini hilo haliwapi woga, badala yake wanahitaji kupambana na kuweka juhudi zaidi katika mchezo huo wa nyumbani.

Gamondi amesema anafahamu misingi ya Mamelodi kwa sababu timu yake ya zamani na wamekuwa bora sana kwa msimu huu, na kwamba waliongeza mchezaji kutoka Argentina kwa usajili ghali tofauti na wao ambao dirisha dogo waliwaleta Joseph Guede na Augustine Okrah wakiwa wachezaji huru.

Amesema kuna tofauti kubwa ya Mamelodi Sundowns na timu kubwa kwa Yanga, ila ni wakati maalum kwao kuonyesha ubora na ili kufikia ukubwa huo wa kuwa miongoni mwa timu tano bora Afrika, lazima wapambane kushinda mechi hiyo.

“Tunahitaji kupigana, kuweka juhudi zaidi kuliko Sundowns, kama nilivyosema awali tulipocheza na Al Ahly, suala la uzoefu lilituathiri kidogo, pia bajeti ukilinganisha na yetu ni tofauti, lazima watu waelewe, lakini haijalishi kwani mpira ni dakika 90 na wote tunacheza 11 dhidi ya 11,” amesema kocha huyo.

Amesema wanatakiwa kuweka juhudi kubwa kuhakikisha wanapambana na timu bora yenye wachezaji wenye uzoefu mkubwa.

Ameongeza kuwa miaka ya hivi majuzi, Mamelodi Sundowns imekuwa ikipata wapinzani wengi kutoka Afrika Kaskazini katika michuano ya Ligi ya Mabingwa, mara ya mwisho kuwa na upinzani Kusini mwa Jangwa la Sahara ilikuwa msimu wa 2021/22 walipotupwa nje na wababe wa Angola, Petro Atletico, hivyo ni zamu ya Yanga kwa kuhakikisha wanashinda mechi ya kwanza ya nyumbani. Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limezikubalia klabu za Simba na Yanga kuwaruhusu nyota wa klabu hizo baada ya mechi ya kwanza ya Fifa Series 2024 dhidi ya Bulgaria itakayocheza Machi 22, mwaka huu, kujiunga na timu zao ili kujiandaa na michezo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo, amesema wamepokea barua kutoka kwa klabu hizo mbili na kuridhia maombi yao ya kutaka wachezaji wao kurejea kwenye vikosi vyao mapema kabla ya Machi 24, mwaka huu ili kupata nafasi ya kujiandaa kuelekea katika michezo hiyo ya robo fainali. 

Simba ina wachezaji wanne katika kikosi cha Taifa Stars ambao ni Aishi Manula, Kennedy Juma, Mohamed Hussein 'Tshabalala' na Kibu Denis huku Yanga nayo ikiwa na Aboutwaleb Mshery, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na Mudathir Yahya.

Akizungumza na Nipashe, Ndimbo alisema katika utaratibu wa tiketi za kurudi tarehe tofauti na wengine, Simba na Yanga wamekubaliwa wachezaji wao kuruhusiwa mapema baada ya mechi ya dhidi ya Bulgaria watarejea nchini na kujiunga na klabu zao.

“Ni kweli Simba na Yanga zilituandikia barua ya kuomba wachezaji wao ambao wako katika kikosi cha kwanza waliopo kwenye majukumu ya Taifa kujiunga haraka kabla ya Machi 25, mwaka huu, ili kuwahi programu ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Al Ahly na Mamelodi Sundowns. 

"Kwa maslahi mapana ya pande zote mbili tumewakubalia, lakini watakuwapo nchini Azerbaijan na kucheza mechi moja dhidi ya Bulgaria baada ya hapo watarejea kuendelea na majukumu ya klabu yao,” amesema Msemaji huyo.