Mkulima jela kwa kuhujumu miundombinu

By Halima Ikunji , Nipashe
Published at 05:39 PM May 07 2024
Ahukumiwa jela kwa kuhujumu miundombinu ya maji.
PICHA: MAKTABA
Ahukumiwa jela kwa kuhujumu miundombinu ya maji.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Igunga mkoani hapa, imemhukumu mkulima, Mohamed Makala (28) kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kuharibu miundombinu ya maji.

Vilevile imemhukumu mkulima mwingine,  Kalolo Wilbati (52) mwaka mmoja jela kwa kukutwa na vitu vya wizi mali ya  Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Igunga (IGUWASA).

Kabla ya hukumu kutolewa, Waendesha Mashtaka wa Ofisi ya Mashtaka Wilaya ya Igunga, Grace Lwila na Albanus Ndunguru kwa nyakati tofauti, walidai mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Edda Kahindi kuwa washtakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya Machi 2 na Mei 2, mwaka jana.

Lwila alidai kuwa mshtakiwa Wilbati alikutwa na vitu hivyo vya wizi zikiwamo mita za maji na mabomba ambavyo vilikuwa vimeibiwa katika maeneo mbalimbali mjini Igunga.

Alidai mshtakiwa Makala anadaiwa kwa makosa matatu ya kuingilia miundombinu ya mifumo ya maji ya IGUWASA na kuiba baadhi ya vifaa.

Mwendesha mashtaka huyo, alidai mshtakiwa huyo alikuwa akiiba vitu hivyo usiku kwa wateja wanaotumia maji ya IGUWASA yaliyounganishwa kutoka Ziwa Victoria na kuacha yakipotea na kuisababishia hasara zaidi ya Sh.milioni 4.4.

Aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa washtakiwa hao kwa kuwa serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kuwekeza sekta ya maji nchini.

Baada ya kusikiliza mashahidi saba wa upande wa mashtaka  na utetezi, Hakimu Kahindi alitoa hukumu dhidi ya washtakiwa hao ili iwe fundisho kwa wengine  wenye tabia ya kuhujumu miundombinu ya maji na kuisababishia serikali hasara.

Hakimu Kahindi alisema mshtakiwa Wilbati atatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kukutwa na vitu vya wizi.

Alisema mshtakiwa  Makala atatumikia kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa matatu.