Madereva bodaboda wapigwa msasa kuzingatia usalama barabarani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:25 PM May 07 2024
Naibu Meya wa Jiji la Dodoma Asma Karama alikabidhi cheti kwa mmoja wa madereva bodaboda wa Jiji la Dodoma baada ya kupata mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva hao.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Naibu Meya wa Jiji la Dodoma Asma Karama alikabidhi cheti kwa mmoja wa madereva bodaboda wa Jiji la Dodoma baada ya kupata mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva hao.

UBALOZI wa Uswisi kwa kushirikiana na shirika la Amend, wamekamilisha awamu ya pili ya mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva wa pikipiki jijini Dodoma.

Baada ya kuhitimu awamu ya pili ya mafunzo hayo, Naibu Meya jiji la Dodoma Asma Karama, leo amekabidhi vyeti kwa madereva 145 waliokamilisha mafunzo hayo yaliyoanza Aprili 15 na kukamilika Mei 4, mwaka huu.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo Mkurugenzi wa Shirika la Amend Tanzania, Simon Kalolo amesema hadi sasa, mradi huo wa usalama barabarani kwa vijana umewafikia madereva bodaboda 398 jijini Dodoma. 

"Katika utekelezaji wa mafunzo haya, shirika la Amend linashirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, viongozi wa serikali za mitaa na shirika la Msalaba Mwekundu, linalowapatia madereva elimu muhimu ya huduma ya kwanza.

"Tunayofuraha tunapohitimisha awamu ya pili ya mafunzo haya hapa Dodoma, kuna mabadiliko makubwa kwani madereva wengi waliopatiwa mafunzo haya wanafahamu Sheria za usalama barabarani pamoja na alama zilizopo Kwetu hili tunasema ni hatua kubwa ya kusaidia kupunguza ajali kwa kundi hili," amesema Kalolo.

Amefafanua kuwa madereva bodaboda waliohudhuria mafunzo hayo wamepatiwa vyeti vya ushiriki pamoja na viakisi mwanga vyenye jumbe mbalimbali wa usalama barabarani.

Ameongeza kuwa katika awamu ya kwanza ya mafunzo hayo, madereva 253 kutoka katika Kata mbalimbali za Jiji la Dodoma zikiwemo Kata ya Uhuru ambako mafunzo haya yamekuwa yakifanyika.

Kwa upande wake,  Mgeni rasmi wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo Naibu Meya Asma Karama amewasihi madereva bodaboda wote waliopata  mafunzo kuwa mabalozi wazuri wa usalama barabarani katika maeneo yao kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Mafunzo haya ya usalama barabarani yaliambatana pia na kampeni ya usalama barabarani kwa vijana na watumiaji wengine wa barabara jijini Dodoma.