Bashungwa atoa siku mbili barabara ya Lindi-Dar ipitike

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 04:37 PM May 07 2024
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo pamoja na Wataalam wengine wakiwa ndani ya Boti katika Bahari ya Hindi wakiwa safarini kutoka Kata ya Somanga kuelekea Mji mdogo wa Kivinje na Kilwa Masoko.
Picha: Mtandaoni
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo pamoja na Wataalam wengine wakiwa ndani ya Boti katika Bahari ya Hindi wakiwa safarini kutoka Kata ya Somanga kuelekea Mji mdogo wa Kivinje na Kilwa Masoko.

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema mpaka kufikia kesho Jumatano usiku au Alhamsi barabara ya Lindi-Dar es Salaam itaanza kupitika.

Mawasiliano ya barabara hiyo yalikatika tangu Jumapili na hivyo kusababisha abiria waliokuwa wakisafiri kuelekea mikoa ya Lindi, Mtwara na Dar es Salaam kukwama.

Akizungumza na wananchi akiwa Nangurukuru wilayani Kilwa ambako ameweka kambi, Bashungwa amesema tayari Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za dharura kwa ajili ya kurejesha mawasiliano ya barabara hiyo.

“Niendelee kuwatoa hofu wananchi na wasafiri wanaotumia barabara hii inayounganisha mikoa ya kusini, tangu jana (juzi)nimepiga kambi huku, nilianzia Somanga na sasa hivi tupo upande huu wa Nangurukuru, kama mnavyoona pande zote wanaendelea na kazi, bado tunaamini ndani ya saa 72, kufikia Alhamisi tutakuwa tumekamilisha kazi ya kurudisha mawasiliano ya barabara hii,” amesema Bashungwa.

Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mohamed Besta kuhakikisha anaongeza idadi ya malori yanayosomba mawe pamoja na mitambo inayotumika kupakia mawe hayo katika magari ili kuongeza kasi ya kujaza vifusi katika eneo la barabara yaliyosombwa na maji.

Bashungwa amesema kuwa pamoja na jitihada za kuagiza makalvati ya plastiki yanayotumika katika dharura za kurejesha mawasiliano ya barabara kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo kwa wakati lakini watalazimika kutumia makontena kwa kuyakata yatumike kama mbadala wa kalvati na kuwezesha maji kupita.

"Niwaambie ukweli wananchi, barabara hizi zimeharibika sana, pale Somanga eneo ambalo maji yalikuwa yanapita, mto umehama na kwenda sehemu nyingine, yamekwenda pia kupasua kwenye uwanja wa mpira,"amesema Bashungwa.

"Kwa hiyo tunahitaji mawe ya kutosha ya kujaza katika eneo la mita nne na la mita 100 na kuweka makaravati, niwahakikishie kwamba kazi hii tunaimaliza ndani ya saa 72 kama tulivyosema kwa kuwa kila kitu tumepata, vifaa tunavyo, mitambo ipo."

Eneo la Barabara lililoharibika ni la mita 80 katika barabara ya Somanga-Mtama ambapo pia tuta la barabara hiyo limekatika katika eneo la Mikereng'ende umbali wa kilomita 10 kutoka Somanga  uelekeo wa Lindi.

Pia, katika eneo la Lingaula nako barabara imekatika kwa umbali wa kilomita 12 kutokea Nangurukuru uelekeo wa Lindi.
Uharibifu wa barabara hiyo ulisabaishwa na mvua kubwa zilizonyesha mwishoni mwa wiki mkoani humo zilizoambatana na upepo mkali.