Vilio vya barabara, maji vyatawala mkutano wa Diwani

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 04:00 PM May 07 2024
Diwani wa Kata ya Bonyokwa Tumike Malilo, akijibu mswali ya wananchi katika kata hiyo alipofanya mkutano wa hadhara kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero.
Picha: Halfani Chusi
Diwani wa Kata ya Bonyokwa Tumike Malilo, akijibu mswali ya wananchi katika kata hiyo alipofanya mkutano wa hadhara kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero.

MKUTANO wa hadhara uliofanywa na Diwani wa Kata ya Bonyokwa, Tumike Malilo umetawaliwa na vilio vya ubovu wa barabara na kukatika kwa maji.

Akifungua pazia la kuwasilisha kero Mkazi wa eneo hilo, Jakobo Jailosi amesema, kero kubwa inayowakabili ni ubovu wa miundombinu ya barabara akisisitiza ni jambo linalokwamisha shughuli za uchumi kwa kiasi kikubwa.

“Barabara ni mbovu, kutoka hapa kwenda Kimara unatumia muda mwingi, ikinyesha mvua ndio balaa hakupitiki kabisa, vivuko kwa maana ya madaraja vimejengwa kwa kiwango cha chini, madaraja mengi hayavukiki na hatujaambiwa lini tatizo hilo litakwisha tunaiomba Serikali itusaidie katika hili” amesema  

Naye Jane Juma, amesema katika kata hiyo kuna changamoto ya kukatika maji mara kwa mara akisistiza ni jambo linalowatesa akina mama.

 â€śMaji yanakatika kila siku na wakati mwingine yanatoka kidogo, Rais Samia Suluhu Hassan alisema lengo lake ni kumtua mama ndoo kichwani lakini hatuoni tunaomba serikali itusaidie kutatua kero hii” amesema   

Akijibu hoja ya kero ya barabara diwani huyo, amesema mwaka huu wamepata fedha za mradi wa kujenga barabara ya kutoka Kinyerezi kupitia Bonyokwa mpaka Kimara, lakini pia ipo ya kutoka Segerea kupitia Magereza mpaka Bonyokwa ambayo nayo ujenzi umeanza na imeshawekwa lami urefu wa mita 700.

Pia amesema barabara ya kutoka Masia mpaka Baampya nayo ipo kwenye mpango wa kujengwa mwaka huu na kawamba kinachosubiriwa ni kupungua kwa mvua zinazo endelea kunyesha.

Kuhusu kero ya maji amesema "Mamalaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DAWASA), wamesema pampu iliyopo ni ndogo kuweza kusukuma maji ili yawafikie wananchi wote kwa wakati lakini wameshaagiza nyingine  mpaka mwisho wa mwezi itakuwa imefika kwahiyo tarajieni kupata maji safi.

"Lakini kubwa zaidi tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan na Mbunge wetu wa Jimbo la Segerea Bona Kamoli kwa kazi kubwa ya kuendelea kulitetea jimbo na kata yetu kwa ujumla, jitihada zao zimezaa matunda na Bonyokwa ya sasa sio ya zamani" alisema huku akishangiliwa na wanachi waliokuwa wamefurika eneo hilo kusikia salamu zake

Afisa Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Sam Swila ameahidi kushirikiana na wana-Bonyokwa kutatua kero zilizo wasilishwa na baadhi ya wananchi katika mkutano huo.

"katika mkutano huu, wapo watu wa DAWASA  kwaajili ya kuelezea kero ya maji pia watu wa TARURA kwaajili ya ubovu wa miundombinu kwahiyo nitasimamia kikamilifu kuhakikisha ahadi na malengo yaliopangwa yanatimia kwa wakati. amesema Mtendaji huyo ambaye alishinda tuzo ya  mfanyakazi bora katika siku ya  sherehe ya Meimosi Mwaka huu.

Katika mkutano huo, Diwani huyo alimwinua Injinia wa TARURA Wilaya Ilala, Fadhili Sadala kutaja mikakati iliyopo kwa wananchi kuhusu ujenzi wa barabara katika kata hiyo naye akajibu: "ipo bajeti imetengwa kwaajili ya ukarabati wa barabara zinazopita maeneo haya tunasubiri mvua ipungue tuanze ujenzi" alijibu 

Akihitimisha mkutano huo Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Omar Kumbilamoto, amesema kata ya Bonyokwa ni miongoni mwa iliyo bahatika kuingia katika Mradi wa Uboreshaji wa Benki ya Dunia akisistiza mradi huo utasaidia kuboresha maeneo mengi katika kata hiyo.

"Kuwapo kwenye mradi huo imetokana na kazi kubwa iliyofanywa na Diwani wenu, bila kumsahahau Mbunge wenu wamepigana kuhakikisha na kata hii inakuwapo kwenye mradi huo" amesema