NBC na SILABU kufikisha elimu ya fedha majumbani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:45 PM May 07 2024
Mwanzilishi Mwenza wa kampuni ya SILABU APP inayotoa huduma za masomo ya ziada kwa wanafunzi majumbani na  kwa njia ya mtandao, Adam Duma akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwanzilishi Mwenza wa kampuni ya SILABU APP inayotoa huduma za masomo ya ziada kwa wanafunzi majumbani na kwa njia ya mtandao, Adam Duma akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo.

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya ushirikiano wa kiutendaji na Kampuni ya SILABU APP inayotoa huduma za masomo ya ziada kwa wanafunzi majumbani na kwa njia ya mtandao. Makubaliano hayo yanalenga kushirikisha walimu wa taasisi hiyo kufikisha elimu ya fedha na huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo kwa wanafunzi wao.

Hatua hiyo inatajwa kuwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwaongezea wanafunzi hao elimu na uelewa kuhusu masuala ya fedha na umuhimu wa kujiwekea akiba tangu wakiwa wadogo.

Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo ilifanyika jana jijini Dar es Salaam ikihusisha mafunzo maalum kwa walimu wa taasisi hiyo yaliyotolewa na maafisa wa benki ya NBC kwa lengo la kuwajengea elimu ya kutosha walimu hao kuhusu huduma na program mbalimbali za benki hiyo mahususi kwa walimu na wanafunzi. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwasaidia vema walimu hao kufikisha elimu hiyo kwa walengwa pindi wanapotimiza majukumu yao.

Akifafanua zaidi kuhusu mpango huo Msimamizi wa Huduma za Elimu wa Benki ya NBC, Yoabu Ndanzi amesema ushirikiano huu utatoa fursa kwa benki hiyo kuweza kuwafikia wanafunzi na walimu kwa urahisi zaidi, hatua ambayo itarahisisha suala zima la kuwajengea uelewa wanafunzi hao kuhusu elimu ya fedha sambamba na kutambua huduma za benki hiyo mahususi kwao.

Huduma hizo ni pamoja na akaunti ya Chanua na akaunti ya wanafunzi (Students Account) mahususi kwa watoto na wanafunzi huku pia walimu wakifikiwa kupitia Akaunti ya Mwalimu iliyobuniwa mahususi kwa ajili yao.

“Ushikiano huu unaboresha zaidi kifurushi cha pamoja kwa maana ya kwamba wakati SILABU wanapeleka darasa nyumbani, NBC pia tunatumia fursa hiyo kuingiza uzoefu wa benki nyumbani na hivyo kuwawezesha wanafunzi kunuafaika na elimu zote mbili ambazo zina umuhimu mkubwa sana kwa maisha yao,’’ amefafanua Ndanzi.

Ameongeza kuwa kupitia mpango huo watoto watawekewa kiasi cha sh elfu 5 kila mwezi kwenye Akaunti zao za Chanua. Fedha hizi zinafadhiliwa na SILABU APP ili kuendeleza ushirikiano na wateja wao ambao ndio wanafunzi kila mwezi.

Akizungumzia ushirikiano huo Mwanzilishi Mwenza wa kampuni ya SILABU, Adam Duma amesema ushirikiano na NBC utahusisha walimu zaidi ya 1,000, utatoa fursa pia kwa walimu hao kunufaika na huduma mbalimbali za vipaumbele zinazotolewa na benki hiyo ikiwemo akaunti ya Mwalimu huku pia kampuni hiyo ikinufaika kupitia matangazo ya huduma zake kupitia majukwaa mbalimbali ya taarifa za benki hiyo.

“Zaidi tunafarijika kuona kwamba sasa ‘package’ yetu ya mafunzo tunayoyatoa kwa wanafunzi wetu inakwenda kuongezewa kitu muhimu sana ambacho  ni elimu ya fedha. Kupitia elimu hii tunakwenda kuandaa kizazi kijacho ambacho kina uelewa wa kutosha kuhusu kujiwekea akiba, kutumia taasisi za fedha kujitengenezea mitaji sambamba na matumizi sahihi ya fedha zao,’’ amesema Duma.

Wakizungumza kwa niaba ya walimu wenzao walioshiriki mafunzo hayo, Mwalimu Sixtmund Byabato na Mwalimu Hellena Mabula pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa kuwapatia elimu hiyo ambayo waliihitaji pia, wamesema mafunzo hayo yamewaongezea uelewa wa kutosha utakaowawezesha kuwafundisha wanafunzi wao. Mafunzo hayo pia yatawasaidia wao katika kufanikisha malengo yao hususani kupitia fursa mbalimbali zitolewazo na benki hiyo kupitia akaunti ya Mwalimu na akaunti ya Malengo huku pia wakitarajia kunufaika na mikopo rasmi ya taasisi hiyo.

Katika hatua nyingine, benki hiyo pia ilitumia fursa hiyo kuzindua msimu wa pili wa program yake ya kimichezo kwa watoto inayofahamika kama 'Chanua Football Kliniki'  itakayofanyika kwenye viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam, Juni 1, mwaka huu.

“Kupitia Chanua Football Kliniki watoto wote wenye akaunti ya Chanua watakuwa na sifa ya kushiriki program hii ya michezo. Vigezo kwa wenye akaunti mpya ni kuwa na ingizo la awali (initial deposit) la kiasi cha Shs 100,000 na kwa wale wenye akaunti hizi tayari kigezo ni kuwa na akiba isiyopungua kiasi cha sh 200,000.’’ 

 â€˜â€™Washiriki (Watoto na wazazi) watapata fursa ya kufurahia michezo na mafunzo mbalimbali, watapata jezi na Zawadi za jumla na za pekee, watashiriki chakula cha mchana pamoja na pia watashiriki michezo na wachezaji mashuhuri wa ligi kuu ya NBC,’’ amesema.