Airtel yaweka rekodi TCRA

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 01:13 PM May 07 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa wa Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh.
PICHA: MAULID MMBAGA
Mkurugenzi Mtendaji wa wa Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh.

RIPOTI ya takwimu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inayotolewa kila robo ya mwaka inayoishia mwezi Machi mwaka huu, imeitaja kampuni ya Airtel kama kinara wa kutoa huduma bora za mtandao.

Kwa mujibu wa ripoti ya TCRA ya mwaka wa fedha 2023/24, Airtel imekuwa mtandao unaongoza kwa kuwa na simu nyingi zilizopigwa kwa robo hiyo ya mwaka  kwa uwiano wa asilimia  38 ya simu za  ndani na 30 kwenda mitandao mingine.    

Aidha, kampuni hiyo imeeleza kuwa hatua hiyo kwao ni uthibisho wa dhamira na mikakati madhubuti iliojiwekea katika kupanua huduma ili kuiweka Tanzania kwenye ulimwengu wa kidigitali.

“Simu nyingi zilizopigwa ndani ya mtandao huo zilichangia asilimia 53 ikilinganishwa na za kwenda mitandao mingine 47. Hii inadhirisha kwamba wateja wa Airtel wanaridhishwa na huduma ambazo zinakidhi mahitaji yao,” imesema sehemu ya ripoti hiyo.

Akizungumzia matokeo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh, amesema ubunifu walionao kwenye huduma na ushindani ndio umewafanya kufikia hatua hiyo, kwa kuwavutia  wateja kuendelea kufurahia kuwa ndani ya mtandao huo.

“Airtel tutaendelea kutoa huduma na masuluhisho mbalimbali ili kuufanya mtandao wetu kuwa nyenzo muhimu katika kuwezesha shughuli za biashara ndani na nje ya nchi,” amesema Balsingh.

Hata hivyo, uchambuzi wa ripoti ya TCRA umeonyesha kuwa  simu zilizopigwa na watumiaji takribani dakika bilioni 35 zilikuwa kwenye viwango bora ndani ya robo ya mwisho ya Machi, ikilinganishwa na dakika bilioni 39 katika robo iliyoishia Desemba 2023.

Vile vile, imebainisha uboreshaji uliofanywa kwenye huduma za mtandao wa Airtel, ikishika nafasi ya kwanza kwa asilimia 97, ikifuatiwa na Halotel 94 na Tigo 94.8. 

Balsingh amesisitiza kuwa Airtel itaendelea na uboreshaji wa miundombinu ya mtandao na kutoa huduma za kibunifu zaidi ili kukidhi mahitaji ya watanzania kupitia mawasiliano. Akieleza kuwa wana nia ya kuendelea kuiunganisha Tanzania kidigtali katika kila jambo linalohitaji huduma za mtandao.