SMZ yaahidi kutatua kero za wafanyakazi kwa wakati

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:57 AM May 02 2024
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
PICHA: MAKTABA
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kutatua kwa wakati changamoto zote za wafanyakazi kwa wakati, ikiwamo kutoa posho ya nauli ya Sh. 50,000 kwa wafanyakazi watakaostahili, kutoa huduma bora kwa wananchi na kuendelea kukuza uchumi wa nchi.

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameyasema hayo kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika Uwanja wa Gombani, Chakechake, mkoa wa Kusini Pemba.

 Pamoja na ahadi hiyo, Rais Dk. Mwinyi ameiagiza  Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, kukutana mara nne kwa mwaka na vyama vya wafanyakazi wakiwamo wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) ili kutatua kwa haraka changamoto za wafanyakazi badala ya kusubiria kila mwaka wakati wa maadhimisho. 

 Dk. Mwinyi amesema serikali pia itaendelea kuwahimiza wafanyakazi kuheshimu na kutekeleza kwa vitendo misingi ya haki za binadamu na utawala bora.

 Amesema iwapo wafanyakazi watazingatia misingi hiyo kwenye utekelezaji wa majukumu yao, ufanisi wa kazi utaongezeka. Pia alisema serikali itazidi kuhakikisha mazingira ya kazi na maslahi ya wafanyakazi yanaimarika ili kuongeza ufanisi kazini.

 Amesema ndani ya kipindi cha  miaka mitano,  serikali imejipangia kutengeneza ajira 300,000 kwa wananchi wake kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 - 2025.

 Ndani ya kipindi cha miaka mitatu, amesema serikali kupitia shughuli mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa barabara, shule, vituo vya afya  na hospitali, bandari, miundombinu ya maji na umeme , ajira mpya 187,651 sawa na asilimia 104 ya lengo la ajira 180,000 zimepatikana.

Kuhusu kuimarisha mazingira bora ya wafanyakazi Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi  amesema, Serikali inaendelea kuimarisha maslahi ya wafanyakazi ikiwemo mishahara, upandishwaji madaraja, nyongeza za mwaka, posho, fidia, nauli kwa wenye kustahiki pamoja na matibabu.  

"Napenda niwahakikishie kuwa serikali ina dhamira ya dhati ya kuendelea kuimarisha mazingira ya kazi na utoaji wa maslahi bora kwa wafanyakazi."  Alisema Rais Mwinyi.   

Katika utekelezaji wa dhamira hiyo, alisema serikali itachukuwa hatua, kuanza kutoa posho la nauli za kwenda kazini na kurudi nyumbani ya Sh. 50,000 kwa watumishi wote wanaostahili kulipwa na kwamba Sh. 34,099,500,000  zimetengwa na Serikali kwa ajili ya posho la usafiri.

Aidha, Serikali imedhamiria kuhakikisha inaongeza fedha kwa ajili ya posho ya likizo na jumla ya Sh. 2,523,814,700 zimetengwa na Serikali kwa ajili ya likizo katika bajeti mpya ya mwaka wa fedha 2024/25.

Amesema, serikali ni sikivu na inaendelea kutoa maslahi na kuimarisha mazingira ya kazi kwa lengo la kuleta ufanisi na maendeleo ya nchi yetu. Pia alisema serikali haitosita kuzitatua changamoto za wafanyakazi na watu wote kwa kadri ya uwezo wake ili kulinda hadhi na heshima yao. 

 Lengo ni kupata maslahi bora ya Utumishi na jamii kwa ujumla kwa kutoa huduma stahiki na kuinua uchumi wa nchi.  

 Kuhusu madeni ya nauli kwa wanaofanya kazi maeneo ya mbali hususani walimu,  Rais Dk. Mwinyi alifafanua baada ya kuondoshwa kwa ugatuzi wa  mwaka 2021 alisema tayari ulipwaji wa nauli hizo umeanza kutolewa kwa walimu wa Skuli za Msingi baadae hatua zitaendelea na kwa walimu wa shule za serikali.

 Akizungumzia suala la wafanyakazi kukatwa kodi nyingi kwenye mishahara yao, kiinua mgongo na pensheni Rais Dk. Mwinyi  amesema serikali kupitia Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji imefanya ufuatiliaji wa hoja hiyo na kubaini kuwa ipo kwa mujibu wa sheria na kanuni za fedha zilizopo. 

Hoja ya kuwepo kwa wafanyakazi wa mkataba wa muda mfupi katika Mabaraza ya Manispaa, Miji na Halmashauri. Tayari suala hili limejadiliwa kupitia vikao vya pamoja na taasisi husika ili kulipatia ufumbuzi, alisema serikali imezitaka taasisi zinazohusika kurekebisha kasoro zilizopo kwa kufuata kwa sheria za kazi. 

Pia amehimiza suala la kudumisha amani, utulivu, maelewano na mshikamano katika sehemu za kazi. Pia alihimiza wafanyakazi wote  kutokufanyakazi kwa mazoea na kuwasihi wajiepushe na rushwa na  ubadhirifu ili uchumi ukue zaidi.

Kuhusu kuimarisha upatikanaji wa ajira za nje ya nchi, Rais Mwinyi  amesema serikali zimejitahidi sana kwenye eneo hilo na serikali ya Tanzania imetia saini mkataba wa ushirikiano na Qatar na Saudia na sasa iko katika hatua za mwisho za kutia saini mkataba na Oman.

Akizungimzia upatikanaji wa ajira hizo,  amesema umeongezeka kwa asilimia 35 kutoka ajira 1,080 kwa mwaka 2022/2023 hadi ajira 3,078 kwa mwaka 2023/24 na ajira za ndani zimeongezeka kwa asilimia 65.9 kupitia mikataba iliyothibitishwa kutoka ajira 6,348 mwaka 2022/23 hadi 9,630 kwa mwaka 2023/24.

Pia amesema kwa serikali kuu, ajira 6,735 zimetolewa kwa watumishi kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Kuhusu uwekezaji, Dk. Mwinyi  amesema ni miongoni mwa vyanzo vya upatikanaji wa ajira za ndani ya nchi na imeimarika.

Akizungumzia miradi mipya iliyotoa ajira, Dk. Mwinyi amesema kwa mwaka wa fedha wa 2023/24, miradi 63 imesajiliwa yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 1,499 na inatarajia kutoa ajira zipatazo 4,392. 

Aidha, amesema serikali ilitoa Sh. bilioni 15 kwa ajili ya programu ya Inuka yenye lengo la kutoa mikopo kwa wajasiriamali na kwa sasa programu hiyo tayari  imetoa mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 22.4 kutokana na fedha za marejesho ambazo zinaendelea kutolewa mikopo mipya na kuzalisha ajira za moja kwa moja kwa wananchi 43,360. 

Kuhusu programu ya Mfuko wa Khalifa (Khalifa Fund) amesema nayo  imetoa mikopo ya Sh. bilioni 2.10 kwa miradi 18 na kuwanufaisha wananchi 19,373 waliojiajiri 

Pia amesema Mfuko wa Bima ya Afya Zanzibar (ZSHF), alisema serikali imeimarisha afya za wafanyakazi na familia zao kwa kuimarisha sheria ya mfuko huo

Amesema hadi kufikia Aprili, mwaka huu, wanachama 48,929 na wategemezi wao wapatao 187,641 walikuwa wamesajiliwa kwenye mfuko huo na kufanya idadi ya wanachama 236,570 hadi sasa.

Akizungumzia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) amesema serikali imetekeleza ahadi kuanzisha mafao mawili mapya kwa wafanyakazi wake likiwamo fao la kuumia kazini na fao la upotevu ajira kwa  wanachama wake wakiwamo wafanyakazi wa sekta zote pamoja na mafao mengine.

Pia  amesema serikali imeanza kuwalipa wastaafu wote kima cha chini cha pensheni kuanzia 180,000.

Kadhalika, kwa kuzingatia wafanyakazi wanaostaafu kwa hiari wakiwa na umri wa miaka 55 watapata  kiinua mgongo kamili badala ya pungufu kama ilivyokua awali. 

Amesema kwa lengo la kuongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa taarifa, Serikali imeanzisha mifumo mbalimbali katika taasisi zake ikiwemo mfumo wa Tehema wa Serikali (e-government) kwa huduma zote za serikali.

Dk. Mwinyi  amesema mfumo mwingine ni Sema na Rais (SNR) wenye lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wakiwemo wafanyakazi wa Taasisi mbalimbali za umma na binafsi. 

Amesema malalamiko 1,903 ya wafanyakazi yamepatiwa ufumbuzi, sawa na asilimia 97 ya malalamiko yaliyowasilishwa yakihusisha madai ya posho, marekebisho ya mishahara na mafao ya kiinua mgongo. Jumla ya Sh. bilioni 3.9 zimetumika kulipa stahiki hizo. 

Aidha, malalamiko 224 yamewasilishwa na wafanyakazi wa sekta binafsi ambapo asilimia 88 kati yao yamepatiwa ufumbuzi. Malalamiko hayo yanahusisha madai ya mishahara, fedha za ZSSF, fidia, wafanyakazi kutokupatiwa mikataba na kutokufuatwa sheria, kanuni na miongozo ya ajira.