Makombora ya Urusi yauwa watano Ukraine

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:34 AM May 02 2024
Mwili wa mtu aliyeuawa katika shambulio la anga la Urusi unaonekana kwenye gari lake Zolochiv, mkoa wa Kharkiv, Ukraine, Mei Mosi, 2024.
Picha: Andrii Marienko/AP/picture alliance
Mwili wa mtu aliyeuawa katika shambulio la anga la Urusi unaonekana kwenye gari lake Zolochiv, mkoa wa Kharkiv, Ukraine, Mei Mosi, 2024.

WATU watano wamefariki dunia baada ya Urusi kufanya mashambulizi katika maeneo ya mashariki mwa Ukraine ya Kharkiv na Donetsk.

DW imeripoti kuwa, Gavana wa eneo la Kharkiv, Oleg Synegubov amesema katika eneo hilo lenye kupakana na Urusi, bomu limeua watu wawili na wengine sita wakijeruhiwa akiwemo mtoto wa umri wa miaka 11.

Pamoja na ripoti za visa vya mauwaji mengine katika eneo la upande wa mashariki zaidi katika mkoa wa Kharkiv karibu na mji wa Kupiansk, makombora ya Urusi yamemua mwanamke wa umri wa miaka 67 katika kijiji cha Lelyukivka.

Eneo hilo ambalo sehemu kubwa zinadhibitiwa na vikosi vya Urusi kwa miezi kadhaa baada ya kuvamia Februari 2022, linakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya Urusi.