USALAMA MAHALI PA KAZI: Simulizi ya utatu wa serikali, mwajiri na mwajiriwa wanavyojitwisha wajibu wao

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:54 AM May 02 2024
Mantiki ya namna usalama mahali pa kazi unavyotekelezwa kwa vitendo.
Picha: Mtandaoni.
Mantiki ya namna usalama mahali pa kazi unavyotekelezwa kwa vitendo.

KILA Aprili 28 ya kila mwaka, dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi, lengo ni kuhamasisha afya na usalama wa wafanyakazi katika maeneo tofauti duniani.

Hiyo pia, ni sehemu ya haki, shukurani na madai ya wafanyakazi, katika siku yao waliosherehekea jana Mei Mosi ya kila mwaka, kama ilivyokuwa jana, kitaifa yakiadhimishwa mkoani Arusha.

 Siku ya Usalama Mahali pa Kazi, ni muhimu kwa taasisi zote, umma na binafsi, kwa sababu sheria za ajira inawabana ziwajibikie taratibu na kanuni zilizowekwa, pia kwa wafanyakazi ambao kwa asilimia kubwa hutumia muda mrefu kazini. Kuwapo  maadhimisho maalum ya siku hiyo, ni muhimu, kwa sababu kila mwaka, inawakumbusha na kuwahamasisha waajiri, kuboresha mazingira yao kazini, ili kuleta ufanisi na kulinda afya na usalama wa wafanyakazi wao. Afya na Usalama Mahali pa Kazi, hutofautiana kati ya sekta moja na nyingine, kutokana na aina ya shughuli zinazofanywa.  

Inaelekezwa, sio kigezo kwa taasisi uzingatia zaidi baadhi ya kanuni na taratibu zilizowekwa kuliko nyingine. Zote zinapaswa kutekelezwa kisheria.

 DK. DOTTO BITEKO

 Katika maadhimisho kitaifa jijini Arusha, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, akawataka waajiri, washirikiane na wadau kuboresha mazingira ya kazi, ili kuongeza usalama mahala kazi.

 Vilevile, inaendana na kuwawezesha watumishi kufanya kazi katika mazingira rafiki, hata kukuza uzalishaji na kupunguza gharama za uzalishaji. "Niwatake waajiri na waajiriwa, kuhakikisha usalama mahali pa kazi, mtu wa kwanza kujali usalama wake ni mwajiriwa. 

 “Ukiona mtambo hauko salama, toa taarifa kwa mwajiri wako; hapa hautaonekana umegoma, bali ni kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama," anasema Dk. Biteko. Akautaka Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), kwa kushirikiana na wadau wa usalama kazini, wanaohakikisha wafanyakazi wanakuwa na mazingira rafiki kuwawezesha kuwa salama, furaha na matumaini wakipata ari kuendelea kufanya kazi na kuongeza ufanisi.

Anasema, pamoja na hatua zinazochukuliwa kutoa elimu, bado inahitajika kuhakikisha pande husika zinaendana na matakwa ya kitaifa na kimataifa. Aidha, anawataka Watanzania kuhakikisha wanakuwa na mkakati wa upandaji miti na nyinginezo, kukabiliana na madhara ya tabianchi, kama vile kuhifadhi vyanzo vya maji. 

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobasi Katambi, anasema serikali inashirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO), kuhakikisha nchi inazingatia usalama na afya kazini.

Mantiki ya namna usalama mahali pa kazi unavyotekelezwa kwa vitendo.
WANAVYONENA WADAU

Meneja wa Masuala ya Afya, Usalama, Ulinzi, na Mazingira (HSSE) wa Asasi ya Puma Energy Tanzania, Ambokege Minga, anaeleza dira ya afya ya kampuni yao ni: "Kuwezesha na kuendeleza wafanyakazi wetu kuwa mstari wa mbele katika masuala ya afya, usalama, ulinzi na mazingira, ili kuziwezesha jamii zetu.

"Hii inamaanisha kwamba tunaendelea kujitolea kila wakati kuendeleza wafanyakazi wanaohusishwa, wanaowezeshwa na wanaoshirikishwa kuweka kipaumbele kuhusu afya na usalama wao, pamoja na wa wengine. “Kila mtu ana haki ya kuwa salama kazini na kurudi nyumbani kwa familia na marafiki akiwa na afya njema kama walivyoanza siku.  

“Tunatambua kwamba kujizatiti kwetu kwa usalama sio tu kuwalinda wafanyakazi wetu bali pia kunachangia mazingira yetu," anasema. Ambokege anaendelea: “Kampuni inaongozwa kwa mujibu wa amali ambazo zinawataka wafanyakazi na washirika wote kuzifuata katika uendeshaji shughuli zetu za kila siku. 

“Tunajivunia kuwekeza nguvu kubwa katika kutoa elimu na kuwahamasisha wafanyakazi kuzingatia masuala ya afya na usalama mahali pa kazi na kuwa mabalozi kwa wenzao nchini kote.  

‘Tumewapatia nguvu ya kusimamia na kutoa taarifa muda na mahali popote ambapo wataona kanuni za afya na usalama zitakapokiukwa,” anaongeza Minga.   Mdau huyo anaeleza, kuzingatia afya na usalama hauishii kwa wafanyakazi pekee, pia makandarasi wanaofanya nao kazi na wageni wanaowatembelea, sehemu zao za kazi. 

Mantiki ya namna usalama mahali pa kazi unavyotekelezwa kwa vitendo.
Lengo analitaja, ni kuhakikisha hakuna anayeumia au kupata madhara, pindi anapofanya nao kazi.   Asasi hiyo inafafanua kwamba, katika juhudi zake inatoa vifaa vya kuwakinga na hatari zinazoweza kujitokeza mahali pa kazi, kama vile vikinga mwili. Pia, asasi hiyo inawahamisha kutoa taarifa, wanapoona sheria zinakiukwa. Kwa mfano, wanapoona mkandarasi anafanya kazi akiwa amevalia vikingamwili, lakini wafanyakazi wake hawana. "Hii inaenda sambamba na kuwatia moyo kutoa taarifa kwa matukio ambayo si salama katika utendaji wa kazi. Matukio haya hutoa mafunzo na elimu kwa wafanyakazi wote ili kudhibiti kutojirudia," anasema na kuongeza:

 “Tunajivunia kuwa mpaka sasa tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufikia malengo makubwa ya masuala ya afya na usalama, kwa sababu hatujapata kesi za ajali au vifo mahali pa kazi, kuanzia mwaka, mpaka sasa hivi.  

“Tunafanya jitihada kubwa katika kutoa elimu, kuwalinda na kuwahamasisha wafanyakazi wetu wote katika shughuli zetu za upokeaji, utunzaji na usafirishaji wa mafuta kwa maendeleo ya wananchi na taifa zima kwa ujumla,” anasema Minga. Mtaalamu wa Udhibiti wa Mazingira ya Usalama wa Afya na Ubora wa kampuni hiyo, Rehema Madoffe, anaeleza kuwa:  “Tunahakikisha wafanyakazi wote wanakuwa na bima za afya bora, ambazo huwalinda pindi wanapokumbwa na changamoto za kiafya.  

“Pia, mahali pa kazi kuna miundombinu imejengwa kwa uthabiti na ubora ili kukabiliana na changamoto mbalimbali kama vile majanga ya moto. 

 “Kwa kuongezea, wafanyakazi hupatiwa mafunzo kukabiliana na majanga ya moto ambapo kila mwezi kwa baadhi ya maeneo yetu ya kazi huwa tunafanya mafunzo ili kujiandaa pindi tunapokumbwa na majanga ya aina yoyote.”  amesema. Maadhimisho ya mwaka huu, 2024 yameongozwa na kaulimbiu ‘Kuangazia Athari za Mabadiliko ya Tabianchi kwa Usalama na Afya Kazini’. Kwa mujibu wa ILO), kaulimbiu hiyo inatokana na uhalisia wa mabadiliko ya tabianchi duniani, yanayoathiri wafanyakazi, kupitia hatari zinazoongezeka, kama vile joto kali, mionzi, mabadiliko ya hali ya hewa, uchafuzi wa hali ya hewa na magonjwa yanayosababishwa na mionzi.