Samatta anavyorejesha kwa jamii kama Sadio Mane

By Saada Akida , Nipashe
Published at 08:32 PM Mar 25 2024
Mwandishi wa Nipashe, Saada Akida, alipomtembelea Mzee Ally Pazi Samatta, kufanya naye mazungumzo maalum.
MPIGAPICHA WETU
Mwandishi wa Nipashe, Saada Akida, alipomtembelea Mzee Ally Pazi Samatta, kufanya naye mazungumzo maalum.

MSHAMBULIAJI wa Al Nassr ya Saudi Arabia, Sadio Mane, ambaye kabla ya kujiunga na timu hiyo alipata mafanikio makubwa akiichezea Liverpool ya England kabla kutimkia Bayern Munich ya Ujerumani, ni miongoni mwa wachezaji wachache wa Afrika wananaojitoa kwa jamii kwa kujitolea kusaidia mambo mbalimbali.

Machache kati ya mengi aliyofanya Mane ni pamoja na kujenga uwanja mkubwa wa kisasa wa soka kijijini kwao, lakini pia akijenga shule za kisasa na hospitali kubwa na siku zote anasema moyoni mwake anafikiria ni namna gani ataweza kuwasaidia zaidi watu wa Senegal.

Ni wanasoka wachache wamekuwa wakijitoa kwa kurejesha katika jamii zao kile wanachokipata, kama ilivyo kwa Mane, mwanasoka wa Tanzania Mbwana Samatta, anayeichezea Klabu ya PAOK ya Ugiriki, naye ameguswa na kuona umuhimu kufanya jambo kubwa kwa jamii inayomzunguka ambapo Ijumaa ya Machi 8, mwaka huu, ulizinduliwa rasmi msikiti aliougharamia kwa fedha zake mwenyewe ukiwa na uwezo wa kuingia waumini 15,000 kwa wakati mmoja.

Msikiti huo uliopewa jina la Masjid Samatta. Upo Vikindu Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, ambapo baba mzazi wa nyota  huyo, Ally Pazi Samatta aliukabidhi rasmi kwa wakazi wa eneo hilo.

Ni Samatta ambaye alianzia soka lake katika Klabu ya Kimbangulile, Mbagala Market kisha African Lyon, Simba, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, KRC Genk ya Ubelgiji na Aston Villa ya England, Galatasaray ya Uturuki na sasa PAOK. 

Nipashe lilifanikiwa kutembelea maeneo ya msikiti huo na nyumbani kwa baba mzazi wa nahodha huyo wa Timu ya Taifa, Taifa Stars kuzungumza mambo mbalimbali ikiwamo wazo lake la kujenga msikiti huo.

MSIKITI UMEKAMILIKA

Mzee Samatta anasema, ana furaha kubwa kuona kijana wake amerudisha shukrani kwa Mungu  na jamii, anaamini kupitia hilo ataendelea kupata baraka kwenye jukumu lake kama mwanasoka.

“Ni jambo jema kumkumbuka Muumba kwenye ujana wake, pamoja na neema anazozipata maishani mwake bila Mungu ni bure, ndio maana akiniambia anataka kufanya vitu vya huduma kwa wengine na kuwa mstari wa mbele kuvisapoti,” anasema Mzee Samatta  na kuongeza 

"Samatta si muongeaji, lakini anajitoa sana kwa jamii bila kubagua, hilo linanigusa kama mzazi, kuna wengine nimewasikia wakisema sasa angekujengea ghorofa, nawaambia ninalo la kwangu nililojenga kwenye ujana wangu, hivyo anachokifanya ni bora zaidi.” UJENZI ULIVYOANZA:

Baba mzazi wa mchezaji huyo anasema kuna siku alitoka Vikindu ambapo kuna viwanja vyake wakati huo Samatta akiwa anacheza TP Mazembe ya DR Congo.

“Nakumbuka ilikuwa mwaka 2017 aliporudi Congo akanieleza anataka kununua viwanja Vikindu kwa ajili ya kujenga nyumba yake ya makazi, nilifanikiwa hilo kwa kupata viwanja hivyo na kununua, lakini baada ya muda mfupi alinifuata na kunieleza amepata kiwanja Kigamboni anataka kununua.

"Nilimkubalia kwa bahati nzuri aliponunua Kigamboni akapata wazo la kujenga nyumba ya kuishi huko na kunieleza kuwa kiwanja cha Vikindu anataka kujenga msikiti.

"Nilimuunga mkono kwa sababu amefuata nyayo za babu yake mmoja anaitwa Mbwana Samatta alijenga nyumba ya ibada huko Bagamoyo,” anasema Mzee Samatta.

Anaelezea kuwa baada ya kuona sijampinga wazo lake akaanza ujezi kwa haraka, umechukuwa muda wa miaka mitatu ujezi ukasimama kwa sababu ya piLika za usajili wake wa kwenda Aston Villa. 

Anasema baada ya kusimama mwaka 2023 wakazi wa Vikindu walimfuata kuomba idhini ya kutaka kutumia msikiti huo, ambapo aliwaeleza hujakamilika ikiwamo kutokuwapo maji pamoja na kutopakwa rangi.

"Waliniomba kutumia hivyo hivyo hadi hapo tutakapokuwa tayari na tukawaruhusu kutumia wakati ujezi ukiendelea hadi umekamilika na kufunguliwa,” anasema baba mzazi wa Samatta.

Msikiti huo wa Samatta ulianza kujengwa mwaka 2017 na  Mzee Samatta anasema ameona kama ametua mzigo kwa kuzinduliwa na kuanza kutumika na roho yake ina amani kubwa.

“Thamani halisi ya msikiti huo hajaiwekwa wazi kutokana usiri mkubwa ambao anao kijana wangu, ni kuwa msiri katika mambo yake mengi,” anasema mzee Samatta ambaye enzi za ujana wake naye alikuwa mahiri katika soka kama ilivyo kwa mwanawe.

 JAMII ANAYOISAIDIA

Mzee Samatta anaeleza kuwa mbali na msikiti huo pia anawadhamini watoto yatima katika vituo viwili (majina hayafahamu), vilivyo Kinondoni na kingine Bagamoyo kwa kuwapa vitu vyote vya msimgi ambavyo wanatakiwa kupata kutoka kwa wazazi au walezi wao.

“Mwaka jana katika mashindano aliyoyaanzisha yeye na Ali Kiba (Samakiba Foundation), alitoa milioni 100 kwa ajili ya kununua vifaa vya akina mama wanaojifungia watoto njiti katika Hospita ya Kibiti ambapo nimezaliwa baba yake,” anasema mzee Samatta.

 VITEGA UCHUMI VYAKE

Baba mzazi wa nyota huyo anasema Nahodha huyo wa Taifa Stars amekuwa na biashara nyingi ikiwamo Samatta Safari Tours kwa ajili ya usafirishaji wa watalii kwenda kutembelea mambo ya kitalii.

“Hajaishia hapo lakini aliniambia anamipango ya kumiliki TV yake kwa ajili ya michezo tu, lakini hajaweka wazi juu ya atakapomaliza soka lake anahitaji kufanya nini."

 AMGOMEA SAMATTA:

Anasema kipindi ambacho Samatta amemaliza nyumba yake, kijana wake alimtaka akaishi Kigamboni, lakini alimgomea kwa sababu hawezi kukaa sehemu ambayo haina makelele wala fujo.

“Nilimkatalia nikamwambia hawezi kuniamisha Mbagala na kwenda kunifungia Kigamboni hutoki nje muda wote ndani hayo maisha ya kizungu siyawezi nimezoea kwangu hapa Mbagala muda wote fujo kelele na kutoka kwenda katika viwanja mbalimbali kuangalia mpira,” anasema Mzee Samatta.