Dk. Ashatu Kijaji mgeni rasmi maadhimisho miliki bunifu

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 03:35 PM May 08 2024
Mkurugenzi wa Miliki Bunifu wa Wakala wa Usajili wa  Biashara na Leseni (BRELA) Loy Mhando akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake kuhusu siku ya miliki bunifu duniani inayoadhimishwa leo. Kushoto ni  Afisa Habari Mkuu Theresia Chilambo.
Picha: Joseph Mwendapole
Mkurugenzi wa Miliki Bunifu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Loy Mhando akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake kuhusu siku ya miliki bunifu duniani inayoadhimishwa leo. Kushoto ni Afisa Habari Mkuu Theresia Chilambo.

WAZIRI wa Viwanda na Bishara, Dk. Ashatu Kijaji anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kongamano la maadhimisho ya siku ya miliki bunifu duniani linalofanyika kesho jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na  Mkurugenzi wa Miliki bunifu wa BRELA, Loy Mhando, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Miliki Bunifu yanayofanyika kesho.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘miliki ubunifu na malengo ya maendeleo endelevu: Kujenga mustakabali wa pamoja kwa kutumia ubunifu’.

Amesema Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO), lilianzishwa kwa lengo la kukuza na kulinda haki wa wabunifu na kulinda alama zilizowekwa kwenye bidhaa au huduma, haki miliki na hakishiriki.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa WIPO hivyo imekuwa ikiunga mkono na kushiriki katika jitihada zinazofanywa na shirika hilo kwa kuhakikisha kuwa inakuza uelewa wa masuala ya miliki bunifu pamoja na kuzilinda kisheria ili kwenda sanjari na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ili kukuza uchumi,” amesema

Amesema katika maadhimisho ya mwaka huu BRELA imewaalika wadau mbalimbali pamoja na taasisi mbalimbali zinazosimamia miliki bunifu Tanzania Bara na Zanzibar, taasisi za umma na taasisi binafsi ili kujadili kwa pamoja fursa, mafanikio na changamoto zilizopo.

Amesema kuelekea maadhimisho hayo, maofisa wa BRELA wametoa elimu kuhusu miliki bunifu katika vyombo mbalimbalivya habari na kuwahamasisha wabunifu kuendeleza na kulinda bunifu zao ili ziwapatie manufaa wao binafsi na taifa kwa ujumla.

“Kutakuwa na mjadala kuhusu miliki bunifu ambayo itahusisha sekta binafsi na za umma ambao kwa pamoja watajadili kuhusu fursa, mafanikio na changamoto wanazokutana nazo katika sekta hii na tutasaini makubaliano ya ushirikiano na baadhi ya taasisi zinazohusika na miliki bunifu ili kuhakikisha miliki bunifu inakuwa na manufaa katika maendeleo ya kiteknolojia na kiuchumi,” amesema

Amesema BRELA imeanza kampeni ya kutoa elimu kwa umma kuhusu miliki bunifu baada ya kubaini kuwa wananchi wengi hawafahamu vyema kuhusu miliki bunifu hivyo wamepanga kuwafikia watu wengi ili waweze kuwa na ufahamu kuhusu miliki bunifu.

“Tumekwenda vyuo vikuu, tumeongea na wawekezaji na wajasiriamali na tunaushirikiano na Tume ya Sayansi na Teknolojia  COSTECH ili kuwafikia wabunifu wa teknolojia za aina mbalimbali kwasababu tume hiyo inaangalia teknolojia na ubunifu,” amesema

Amesema kupitia ushirikiano huo wameshatambua teknolojia zilizovumbuliwa na vijana kwenye mikoa mbalimbali ambako wametambua teknolojia za vijana 25 na BRELA imewashauri waziweke kwenye namna ambayo italeta sukuhisho la matatizo mbalimbali ya kijamii.

“Lakini tunahakikisha bunifu zao zinapatiwa ulinzi na kuzuia watu wengine kuzitumia bila ridhaa yao na hali hii inampa moyo mbunifu aendelee kubuni vitu vingine zaidi kwasababu anajua kazi zake zitalindwa na wakala,” amesema

Amesema mkakati mwingine wa wakala ni kuwapa elimu waandishi wa habari ili waweze kutambua haki za wabunifu na kwamba mpaka sasa wameshawapa mafunzo waandishi 160 kutoka vyombo mbalimbali.