Kiama wauza mafuta kwenye vidumu

By Neema Sawaka , Nipashe
Published at 12:47 PM May 08 2024
Wauza mafuta kwenye vidumu watangaziwa vita.
Picha: Maktaba
Wauza mafuta kwenye vidumu watangaziwa vita.

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA ) Kanda ya Magharibi, inatarajia kuanza msako wa wafanyabiashara wa mafuta kwenye vidumu na mapipa hivi kwa kukiuka sheria na kuhatarisha maisha ya wananchi.

Msako huo umetangazwa na Meneja wa EWURA  wa Kanda hiyo, Walter  Chirstopher,  wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa ili kudhibiti biashara hiyo na madhara yake katika jamii.

Christopher amesisitiza kuwa wafanyabiashara hao wa mafuta aina ya petrol, diseli na taa wanatakiwa kutambua kuwa siku zao zinahesabika na kuonya kuwa wakikamatwa watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kukiuka sheria za mamlaka hiyo na kuhatarisha maisha ya wananchi kwenye maeneo yao.

“Sheria  ya mafuta  ya mwaka  2015 kifungu  cha  131 inasema  mtu yoyote  haruhusiwi kuuza mafuta hayo bila kuwa na leseni  kutoka  EWURA,” amesema na kufafanua kuwa: “ Masharti ya EWURA mfanyabiashara anayotakiwa kutimiza ni kuwa na leseni na kujenga  kituo   cha  mafuta." 

Mhandisi  Mwandamizi wa Mafuta wa EWURA, Ibrahimu  Kajugusi,  amesema mamlaka hiyo imepunguza masharti ya kuanzisha biashara hiyo na kwamba taratibu  ziko wazi kwa mfanyabiashara anayetaka gharama za uanzishwaji vituo kwa vijijini zimeainishwa.

“Kwa taarifa ya Aprili 30, mwaka huu tulikuwa na vituo vya mafuta 464 vilivyojenga vijijini nchini nzima kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi na kuondokana na biashara ya kuuza mafuta kwenye chupa za maji ndani ya makazi ya watu, tunaendelea kuweka mazingira wezeshi ili viendelee kujengwa zaidi,” amesema.