Askari wanaovujisha siri za wananchi waonywa

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 10:42 AM May 08 2024
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Singida, Amon Kakwale.
Picha: Maktaba
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Singida, Amon Kakwale.

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Singida, Amon Kakwale, ametoa onyo kwa askari yeyote mkoani hapa atakayebainika kutoa siri anazopewa na raia, kusababisha madhara kwa mtoa taarifa.

Amesema hatua zitazochukuliwa kwa atakayebainika ni pamoja na zile za kinidhamu ikiwamo kufukuzwa kazi.

Ametoa onyo hilo katika kikao alichokiitisha cha wadau wa ulinzi na usalama wa Manispaaa ya Singida kwa ajili ya kujitambulisha kwao baada ya kuripoti mkoani Singida akitokea mkoa wa kipolisi wa Temeke jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho ambacho pamoja na mambo mengine kililenga kuweka mikakati ya kuimarisha ulinzi.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wenyeviti wa serikali za mitaa, viongozi wa vyama vya siasa, madiwani, wafanyabiashara, viongozi wa dini na wa masoko yaliyopo Manispaa ya Singida.

Baadhi ya washiriki wa kikao hicho wamedai kuwa wakati mwingine wananchi wanakuwa wagumu kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kutokana na baadhi ya askari wasio waaminifu kuvujisha siri wanazopewa.

Kufuatia hali hiyo, Kamanda Kakwale amesema ili Jeshi la Polisi liweze kupata mafanikio katika utendaji kazi wake askari wanatakiwa kuwa na nidhamu, kutenda haki, weledi na uadilifu.

Amesema tukio la hivi karibuni la walinzi wawili waliouawa maeneo ya Stendi Kuu ya Mabasi Singida lilikuwa ni sawa na Jeshi ka Polisi kupigwa za uso.

Amesema suala la kulinda raia na mali zao ni jukumu la kila mwananchi, hivyo kinachotakiwa ni kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za matukio ya uhalifu. 

Kakwale amesema kwa kutambua kuwa Jeshi la Polisi pekee haliwezi kufanya chochote mwaka 2006 lilikuja na mfumo mpya wa ushirikishwaji wa jamii, kuwa na mkakati wa polisi kata lengo likiwa ni kusogea karibu na wananchi.