Mafuriko yaja na kipindupindu Kenya, 44 waugua

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:48 PM May 08 2024
Wagonjwa wa Kipindupindu wameripotiwa katika Kaunti ya Tana River Kenya.
Picha: Thomas Mukoya/REUTERS
Wagonjwa wa Kipindupindu wameripotiwa katika Kaunti ya Tana River Kenya.

TAKRIBAN wagonjwa 44 wa kipindupindu wameripotiwa katika kaunti ya Tana River nchini Kenya, huku mafuriko yakiongeza hatari ya kuenea kwa maradhi hayo yanayotokana na maji.

Shirika la Afya Duniani (WHO), limesema Kaunti ya Tana River ni moja ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko.

Mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya, Stephen Jackson, katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni, amesema anaamini kuwa kwa ushirikiano kati ya serikali na washirika wa kitaifa na kimataifa, watafanikiwa kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Afya wa Kenya, Mary Muthoni amesema kuna hatari kubwa ya magonjwa yanayosambazwa na maji kuwa janga ikiwa hayatashughulikiwa kwa wakati.
 
Muthoni na maofisa wengine wa afya wamesambaza bidhaa za kusafisha maji katika mji mkuu, Nairobi.

Kulingana na takwimu za hivi karibuni zilizochapishwa na vyombo vya habari vya ndani, mafuriko nchini Kenya yamesababisha vifo vya watu 238 huku zaidi ya watu wengine 200,000 wakiwachwa bila makao rasmi.