Bilioni 3.9 yatolewa na Airtel kwa watanzania

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 05:14 PM May 08 2024
Mkurugenzi wa Airtel Money Andrew Rugamba.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Airtel Money Andrew Rugamba.

SH. Bilioni 3.9 zimetolewa na Airtel kama gawio la faida itakazogawanywa kwa wateja na mawakala wa wake nchi nzima ambao wamekuwa wakitumia huduma hiyo kuanzia Julai hadi Desemba 2023.

Imeelezwa kuwa utoaji wa fedha hizo ni uthibitisho wa kuendela kufanikiwa kwa mikakati ya kampuni hiyo katika kuboresha huduma za kifedha kupitia ili kutoa huduma bora, zenye ubunifu na nafuu kwa watanzania.

Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Airtel Money Andrew Rugamba, amesema fesha hizo hutolewa kila robo ya mwaka, akieleza kuwa kampuni hiyo ilianza kugawa gawio la faida tangu mwaka 2015 ambako hadi sasa imeshagawa jumla ya Sh. bilioni 52 kwa wateja na mawakala wake nchini nzima.   

"Airtel tutaendea kutekeleza dhamira yetu ya kutoa huduma nafuu na kuleta mifumo bora ya kupanua miundombinu ya huduma zetu ili kuendelea kusambaa na kutoa huduma vijijini na mjini, pia tutaendelea kupanua zaidi mtandao wa mawakala ili kuhakikisha huduma zote zinapatikana kwa urahisi kwa wananchi walio wengi," amesema Rugamba.

Amesema hadi sasa kampuni hiyo ina zaidi ya matawi yanayotoa huduma za fedha 4,000 na mawakala 250,000 nchi nzima, pamoja na kujiunganisha na mifumo ya malipo kielektroniki, ikiwemo ya serikali ili kuwawezesha wateja kufanya malipo mbalimbali ya serikali wakiwa popote.

Aidha, amebainisha kuwa wameunganishwa na zaidi ya benki 40 nchini, jambo litakalowawezesha wateja wao kufanya miamala ya kifedha kutoka kwenye akaunti zao za benki kwenda kwenye akaunti zao za Airtel kwa urahisi.

Hata hivyo, amesema Airtel inaendelea kujizatiti katika kuboresha huduma za kifedha kupitia simu kwa wateja wake na itandelea kubuni huduma mbambalia kutokana na mahitaji ya wateja wake na watanzania kwa ujumla ili kuendelea kutoa suluhisho la huduma za kifedha kidijitali na kuondoa changamoto ya kutofikiwa na huduma za kifedha popote nchini.