Vipaumbele vitano sekta ya elimu 2024/25

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 02:37 PM May 08 2024
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, akiwasilisha Hotuba ya  ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, bungeni  jijini Dodoma.
PICHA: IBRAHIM JOSEPH
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, akiwasilisha Hotuba ya ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, bungeni jijini Dodoma.

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanika vipaumbele vikuu vitano kwa 2024/25 vinavyolenga kuleta mageuzi katika sekta ya elimu, kikiwamo ujenzi wa shule mpya 100 za sekondari za ufundi ambazo 26 kati ya hizo, zitaanza kupokea wanafunzi kuanzia Januari, mwakani.

Pia imesema serikali itaongeza fursa za utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wenye sifa na uhitaji kutoka 223,201 hadi 252,245 na wanafunzi 84,500 wa mwaka wa kwanza watanufaika. Pia wamo wa shahada ya kwanza 80,000, shahada za juu 2,000, wanaosoma nje ya nchi 500 na Mfuko wa Ufadhili ya Samia (Samia Scholarship) 2,000 na wanafunzi 157,745 wanaoendelea na masomo.

Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka 2024/25, Waziri Prof. Adolf Mkenda ameliomba Bunge kupitisha Sh. trilioni 1.96 ili kutekeleza vipaumbele hivyo, vinavyolenga kuimarisha ubora wa elimu ili vijana wapate maarifa, ujuzi, kujiamini, kujiajiri na kuajirika.

Prof. Mkenda ametaja vipaumbele vingine kuwa ni kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji  elimu na mafunzo nchini na pia kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya  ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (amali na amali sanifu), kuimarisha ubora wa elimu ya  msingi, sekondari na ualimu.

“Kipaumbele kingione ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya  juu na kuendeleza utafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu,” amesema.

MABORESHO MITAALA

Amesema kwa mwaka ujao, serikali itafanya mapitio ya mitaala 171, kuandaa mitaala mipya 18, kuanzisha programu za vipaumbele 145 na matumizi ya mbinu bunifu za ufundishaji katika elimu ya juu.

Serikali, amesema itaanzisha vituo vya elimu huria (OER) ili kuimarisha majukwaa ya ndani na kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu; itasasisha na kuandaa mtaala mpya katika taasisi 17 za elimu ya juu na itahakiki mitaala 230 ya vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

“Lengo ni kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakidhi mipango ya nchi, soko la ajira la kitaifa na kimataifa na kuwawezesha wahitimu kujiajiri na kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira,” amesema.

“Serikali pia itaandaa mwongozo wa elimu jumuishi wa ufundishaji na matumizi ya teknolojia kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ufundishaji na  matumizi ya teknolojia katika elimu na mafunzo; itafanya mapitio ya mwongozo wa uanzishaji na usajili wa shule wa mwaka 2020 ili kuendana na mabadiliko ya sera na mitaala,” amesisitiza.

kadhalika, amesema itakamilisha mwongozo wa kuwatambua na  kuwaendeleza wanafunzi wenye vipawa na vipaji; itaandaa kiunzi, mwongozo na zana kwa ajili ya  kuwezesha upimaji wa ujifunzaji kwa wanafunzi katika ngazi husika.

UFUNDI NA UFUNDI STADI

Amesema ujenzi wa shule hizo mpya za amali (ufundi na ufundi stadi) utapewa  kipaumbele katika maeneo ambayo hayana vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi  au shule ya amali ya sekondari.

“Serikali itasajili vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi 150 ambapo vyuo vya elimu ya ufundi ni 100 na vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi    50, hivyo kuwa na jumla ya vyuo 504 vya elimu ya ufundi na vyuo 885 vya mafunzo ya ufundi stadi,” amesema.

Amesema usajili wa taasisi hizo utawezesha kuongeza fursa na kutoa mafunzo kwa kuzingatia viwango na ubora.

Amebainisha kuwa wanafunzi 263,718 watadahiliwa wa elimu ya ufundi   na mafunzo na ufundi stadi kati yao wanafunzi  wa vyuo vya elimu ya ufundi ni 190,518 na wanafunzi wa vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi ni 73,200 sawa na ongezeko la asilimia 23 ikilinganishwa na udahili wa mwaka 2023/24.

Amesema udahili unalenga kuongeza rasilimaliwatu yenye ujuzi na uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa.