KenGold kuzipeleka Simba, Yanga, Uwanja wa Chunya

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:36 AM May 02 2024
Mkuu wa Wilaya ya Chunya,  Mbaraka Batenga.
Picha: Maktaba
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbaraka Batenga.

BAADA ya kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya KenGold FC imeazimia kucheza mechi zake kwenye Uwanja wa Chunya uliopo Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya, ambapo Serikali ya Wilaya hiyo na wadau wameahidi kuufanyia maboresho makubwa uwanja huo ili mechi zake zote zikiwemo dhidi ya klabu za Simba na Yanga zichezwe hapo.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya,  Mbaraka Batenga, amesema baada ya KenGold kupanda watafanya kila njia ili kuufanyia marekebisho makubwa kwa ajili ya kuuwezesha kukidhi kanuni za Ligi Kuu.

Akizungumza kwenye hafla ya kuipongeza timu hiyo kupanda Ligi Kuu, Batenga alisema halikuwa jambo jepesi kwani walisubiri misimu minne ili kupata fursa hiyo.

"Halikuwa jambo jepesi, tumesubiri misimu minne mpaka kupanda Ligi Kuu na kuchukua ubingwa wa Championship.

"Sasa kinachoendelea ni kwamba tunataka kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara tukiwa Chunya, tunataka kuileta nchi hapa, kwa hiyo wadau wote tushirikiane kwa pamoja, unajua hii ni fursa kwa wakazi wa huku, kuanzia mama lishe,  wenye nyumba za kulala wageni, mabasi, bodaboda, bajaji, mahoteli makubwa na huduma nyingi muhimu za kijamii, tushirikiane, tukajipange kwa tukio hili la mara ya kwanza kwenye historia ya wilaya yetu, tunakwenda kuhangaika na ule Uwanja wa Chunya hadi kieleweke, ligi ichezwe huku, Simba na Yanga nazo zije," alisema mkuu huyo wa Wilaya.

Wakati huo huo, uongozi wa klabu ya Tanzania Prisons imeipongeza KenGold kwa kupanda Ligi Kuu kutoka Ligi ya Championship.

Taarifa ya Klabu hiyo imesema kuwa kupanda kwa timu hiyo ni fursa nyingine kwa wakazi wa Mbeya kushuhudia burudani kutoka kwa timu hizo mbili za jiji la Mbeya.

"Tunaipongeza KenGold kwa kuwa Bingwa wa Championship, na kupanda Ligi Kuu. Hii ni fursa kwa wakazi wa Mbeya kushuhudia soka safi na burudani kwa timu hizi," ilisema taarifa hiyo ya pongezi.