Yanga yawakomalia nyota wake

By Faustine Feliciane ,, Saada Akida , Nipashe
Published at 10:23 AM May 02 2024
Nickson Kibabage.
Picha: Yanga SC
Nickson Kibabage.

UONGOZI wa klabu ya Yanga umeanza mchakato wa kuwabakisha wachezaji nyota wake wanaowahitaji ambao mikataba yao inaelekea ukingoni.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo inaeleza kwa kuanzia uongozi wa timu hiyo umemalizana na mabeki wake Nickson Kibabage na Shomari Kibwana ambao mikataba yao ilikuwa inaelekea kumalizika.

Kibabage ambaye yupo Yanga kwa mkopo kutoka klabu ya Singida Fountain Gate, amesaini rasmi mkataba wa moja kwa moja wa miaka mitatu kuitumikia timu hiyo.  

Inaelezwa mkataba wa mkopo wa beki huyo unamalizika mwishoni mwa msimu huu lakini kutokana na uwezo aliouonyesha amepewa mkataba huo wa miaka mitatu.

Taarifa za uhakika zilizoifikia  Nipashe jana, ni kuwa Kibabage amesaini mkataba huo akitokea Singida Fountain Gate FC na sasa ni mali rasmi ya Yanga na kuzima ndoto za klabu ya Simba ambayo ilionekana kumhitaji kwa udi na uvumba mchezaji huyo kwa ajili ya msimu ujao.

Imeelezwa kuwa baada ya Simba kuhitaji huduma ya beki huyo na kupeleka ofa yao Singida Fountain Gate FC uongozi wa Yanga uligoma kumuachia na kuamua kupandisha dau na kufanikiwa kumpata na kumsainisha mkataba huo miaka mitatu kusalia ndani ya kikosi cha Yanga.

"Ni kweli Kibabage amesaini mkataba wa miaka mitatu na sasa anaendelea kusalia ndani ya Yanga baada ya kuwepo kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Singida Fountain Gate FC," alisema mmoja wa viongozi wa Yanga.

Baada ya kukamilisha dili hilo tayari wameanza mazungumzo na wachezaji wengine wanaomaliza mikataba yao akiwamo Shomari ambaye anawindwa na klabu ya Azam FC.

Hivi karibuni Rais wa Yanga, Hersi Said alinukuliwa akisema watahakikisha wanamalizana wachezaji wote wanaotaka waendelee kuitumikia klabu hiyo kwa kuwaongezea mikataba.

“Kama tunataka kufanya vizuri ni lazima tuendelee kuwa na wachezaji wetu wenye uwezo mkubwa na kuwaongezea baadhi ili kuendeleza ubora wa kikosi chetu katika Ligi na michuano ya Kimataifa,” alinukuliwa Hersi.

Alipoulizwa Ofisa Habari wa Singida Fountain Gate FC, Hassan Massanza, alikiri kuwapo kwa mazungumzo kati ya uongozi wa Yanga na Singida Fountain Gate ya kumnunua jumla mchezaji huyo.

“Ni kweli hilo jambo lipo, tulipokea ofa kutoka klabu mbili ikiwamo Yanga na wao ndio wameonyesha uhitaji zaidi wa kumnunua mchezaji wetu na tayari tumeshafanya nao mazungumzo, kwa  sasa tupo kwenye hatua za mwisho kukamilisha sehemu iliyobakia,” alisema Massanza.