Simba yaweka rekodi matokeo mabaya zaidi

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:18 AM May 02 2024
Kikosi cha Simba SC.
Picha: Simba SC
Kikosi cha Simba SC.

MABAO mawili iliyoruhusu Simba juzi kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi, imeifanya timu hiyo kuweka rekodi ya kuruhusu mabao mengi kwenye goli lake kwa mara ya kwanza baada ya misimu tisa.

Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu, Simba ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Namungo FC na kujiweka kwenye mazingira magumu ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Timu hiyo imeruhusu mabao 23 mpaka sasa katika mechi 22 iliyocheza, ikiwa ni rekodi mbovu kuwahi kutokea katika mechi zake Ligi Kuu kwa misimu tisa iliyopita.

Mara ya mwisho kuruhusu mabao mengi ilikuwa ni msimu wa 2013/14, ilipomaliza ligi ikiwa imeruhusu mabao 27 katika michezo 26 iliyocheza msimu mzima huku timu 14 zikishiriki ligi katika misimu huo.

Huenda idadi hiyo ya mabao inaweza kufikiwa au kuvunjwa kwani timu hiyo inaendelea kucheza mechi zake za ligi, ikiwa imebakisha mechi nane na takwimu zinaonyesha kuwa bado mabao matano tu ili iweze kuvunja rekodi ya msimu huo ya kuruhusu mabao mengi.

Rekodi zinaonyesha kuwa timu hiyo imekuwa na wastani wa kuruhusu bao moja katika kila mechi mpaka kufikia sasa huku ligi hiyo ikielekea ukingoni sawa na msimu huo wa 2013/ 2014.

Msimu uliofuata baada ya msimu wa 2013/2014, Simba iliruhusu mabao 19 katika michezo 26 iliyocheza huku msimu uliofuata wa 2015/2016 ikiruhusu mabao 17 katika mechi 30.

Wastani wa kuruhusu mabao kwenye lango lake uliendelea kushuka ambapo msimu wa 2017/18 iliruhusu mabao 15 tu katika michezo 30 iliyocheza wakati msimu wa 2018/19 Simba iliruhusu mabao 15 katika michezo 38 iliyochezwa msimu mzima, msimu huo ligi ilishirikisha timu 20.

Msimu wa 2019/20, iliruhusu mabao 21 kwenye wavu, ikicheza mechi 38, 2020/21 na msimu wa 2021/22, iliruhusu mabao 14 uliopita 2022/23, iliruhusu mabao 17.

Takwimu hizo zinaonyesha kikosi hicho ambacho kwa sasa kipo chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mgunda kimekuwa na udhaifu kwenye safu ya ulinzi msimu huu.

Baada ya mchezo wa juzi dhidi ya Namungo FC, Mgunda alikiri kuwapo kwa mapungufu makubwa kwenye timu hiyo.

"Kuna kazi ya kufanya kwenye safu ya ulinzi, tunaruhusu mabao mepesi, mabeki wamekuwa na makosa, hawana mawasiliano na unaweza ukaona hata goli tuliloruhusu na Namungo kusawazisha," alisema Mgunda na kuongeza,

"Inauma, inagusa, lakini siku zote mchezo wa mpira ni mchezo wa kikatili kwa hiyo lazima tukubaliane nayo, pia tumejifunza kitu, tutaenda kukaa chini kutafakari kuona yale yaliyojitokeza, lazima tuweke mambo sawa, safu ya ulinzi lazima iwe imara,” alisema Mgunda ambaye ilikuwa ni mechi yake ya kwanza, baada ya kuondoka aliyekuwa Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha raia wa Algeria.

Kwa matokeo hayo, Simba imeendelea kuwa nafasi ya tatu, ikiwa na pointi 47 na kutishia ushiriki wake kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambako wamekuwa wakishiriki mfululizo kwa misimu saba.

Ili kuweza kucheza Ligi ya Mabingwa, Simba italazimika kushinda mechi zake zote zilizobaki, ikiwamo dhidi ya Azam FC, Mei 9.

Kwa msimamo ulivyo na mechi zilizobakia, kama Simba atashinda mechi zake zote zilizobakia (ikiwamo dhidi ya Azam FC), itafikisha pointi 71 na kama Azam itashinda mechi zake zote (ikiwamo dhidi ya Simba) itafikisha pointi 72.