Bei ya mafuta petroli yapaa, dizeli yashuka

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 09:18 AM May 02 2024
Bei ya mafuta petroli yapanda.
PICHA: MAKTABA
Bei ya mafuta petroli yapanda.

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei mpya za mafuta zilizoanza kutumika jana huku bei ya rejareja ya petroli ikiongezeka kwa Sh. 57 kulinganisha na mwezi uliopita na dizeli ikishuka kwa Sh. 14.

Taarifa ya mamlaka hiyo ilieleza kuwa mabadiliko ya bei za mafuta kwa Mei ,2024 yamechangiwa na ongezeko la bei za petroli iliyosafishwa katika soko la dunia (FOB) kwa wastani wa asilimia 3.90 na kupungua kwa wastani wa asilimia 1.31 kwa mafuta ya dizeli.

Imetaja sababu nyingine kuwa ni kupungua kwa gharama za uagizaji mafuta  kwa wastani wa asilimia 7.21 kwa petroli na asilimia 2.15 kwa dizeli kwa Bandari ya Dar es Salaam, asilimia 10.14 kwa petroli na asilimia 23.18 kwa dizeli kwa Bandari ya Tanga na wastani wa asilimia 5.32 kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa Bandari ya Mtwara.

“Aidha, mabadiliko hayo yamechangiwa na kubadilika kwa kiwango cha kubadilishia fedha za kigeni na kuendelea kutumia ‘EURO’ kulipia mafuta yaliyoagizwa,” imeeleza sehemu ya taarifa ya EWURA.

Taarifa hiyo imeonyesha kuwa bei ya jumla ya mafuta yanayochukuliwa katika Bandari ya Dar es Salaam, petroli imepanda  hadi kufikia Sh. 3,181.48 kwa lita kutoka Sh. 3,125.27 iliyotangazwa mwezi uliopita, huku dizeli ikishuka hadi Sh. 3,063.68 kutoka Sh. 3,077.94.

Kwa mkoa wa Tanga, bei ya jumla ya petroli sasa itauzwa Sh. 3,184.05 kutoka Sh. 3,129.50 na dizeli Sh. 3,069.46 kutoka Sh. 3,085.59. Mkoa wa Mtwara petroli itauzwa Sh. 3,185.05 kutoka Sh. 3,128.03 na dizeli Sh. 3,067.90 kutoka Sh. 3,079.23.

Kutokana na  hali hiyo, bei ya rejareja ya petroli kwa Dar es Salaam imepanda kwa  Sh. 57 huku dizeli ikishuka kwa Sh.14, hivyo petroli kwa rejareja kwa mkoa huo  sasa itauzwa Sh. 3,314   kutoka Sh. 3,257,  huku dizeli ikiuzwa Sh. 3,196  kutoka Sh. 3,210 .

Katika mkoa wa Tanga, bei ya rejareja  ya petroli sasa ni Sh. 3,360 kutoka Sh. 3,303 huku dizeli ikiuzwa Sh. 3,242 kutoka Sh. 3,256. Mtwara, petroli ni Sh. 3,317 kutoka Sh. 3,260 na dizeli inauzwa Sh. 3,200 kutoka Sh. 3,212.

Taarifa hiyo imeonyesha bei ya bidhaa hizo rejareja kwa sasa kwa mikoa mingine ikiwamo Arusha ambayo petroli ni  Sh. 3,398 huku dizeli ikiuzwa Sh. 3,280, Mara  Petroli ni Sh. 3,479 na Dizeli Sh. 3,362, na Sumbawanga mkoani Rukwa   Petroli  ikiuzwa Sh. 3,487  na dizeli Sh. 3,369.