Yanga yaanika siri inapowazidi Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:58 AM Oct 14 2024
Meneja wa Yanga, Walter Harrson.
Picha:Mtandao
Meneja wa Yanga, Walter Harrson.

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga imetamba sababu kubwa inayowapa ushindi katika mechi za dabi kwa siku za karibuni ni kutokana na kikosi chake kuundwa na wachezaji wengi wazoefu na wanaotambua umuhimu wa michezo hiyo.

Yanga itashuka ugenini katika mechi ya watani wa jadi ya mzunguko wa kwanza itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Meneja wa Yanga, Walter Harrson, aliliambia gazeti hili uwezo na juhudi za wachezaji wao ambao wanajipanga kucheza katika viwango vya juu pamoja na kuonyesha 'vitu' walivyonavyo mbele ya mashabiki wao husaidia kupata matokeo chanya.

Harrison alisema wao kama viongozi linapokuja suala la mechi ya dabi huwa hawazungumzi sana kwa sababu mechi yenyewe inajieleza na kila mchezaji anajiandaa vyema kisaikolojia kutimiza majukumu yake.

Meneja huyo alisema kila mchezaji anajua anachotakiwa kukifanya katika mchezo huo na wanafahamu kiwango bora huwasaidia kujiongezea thamani na umaarufu lakini wakijua pia wanajiweka sokoni.

"Tumekuwa tukipata ushindi kwa siku za hivi karubuni tukicheza dhidi ya Simba, kikubwa kwetu viongozi mechi hii hatuhitaji kuhamasisha sana kama michezo mingine ambayo wachezaji wanakuwa wamejisahau au wanazichukulia kawaida. 

Kwa kiasi kikubwa wachezaji wetu wengi wameshacheza mechi hizi, hawahitaji sana kuelezwa, hakuna asiyefahamu ukubwa wa dabi. Wenyewe wanajiandaa na kila mmoja anataka kupata nafasi ili aonyeshe alichonacho akijua ataangaliwa na watu wengi uwanjani na kupitia televisheni, kwa hiyo haiitaji sana kuizungumza, yenyewe inajizungumza," alisema Harrison.

Kuhusu maandalizi, meneja huyo alisema wanaendelea na mazoezi na kufanyia maboresho makosa ambayo waliyabaini katika michezo iliyotangulia ili kuhakikisha wanaendeleza ubabe dhidi ya Simba.

"Tuko katika maandalizi makali, tunaweka kila juhudi inayotakiwa kuhakikisha tunashinda. Huu ni mchezo mkubwa unaobeba hisia, lakini una pointi tatu tu, utofauti ni uhasimu tu uliopo, hii ni ligi yenye michezo 30, hata kama tukishindwa kupata matokeo mazuri, tunaweza kucheza mechi nyingine tukashinda, tukawa mabingwa," meneja huyo aliongeza.

Alisema pia suala la kuwapa ahadi endapo watashinda mechi hiyo kwao hufanyika katika kila mchezo lakini ni huwa ni siri baina ya klabu na wachezaji.

"Sisi kila mchezo tunahamasishana wenyewe kwa wenyewe na ahadi huwa ni siri, si tunafanya katika mchezo huu wa dabi, bali ni kwa ligi nzima, kila mechi kwetu ni muhimu," alifafanua Harrison.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana katika mechi ya hatua ya nusu Fainali ya Ngao ya Jamii iliyochezwa Agosti 8, mwaka huu, Yanga ikishinda bao 1-0 shukrani kwa Mkongomani, Maxi Nzengeli.

Yanga ambayo ina pointi 12, imecheza mechi nne mpaka sasa iko katika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara inayoshirikisha timu 16 kutoka mikoa mbalimbali.

Watani zao Simba wamejikusanyia pointi 13 baada ya kucheza michezo mitano wakati vinara wa ligi hiyo ni Singida Black Stars yenye pointi 16 lakini imeshuka dimbani mara saba.

Ligi hiyo ilisimama kupisha Kalenda ya Kimataifa, ambapo kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa wenyeji Taifa Stars wataikaribisha Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo), katika mechi ya Kundi H ya kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025).