Minziro atua rasmi Pamba Jiji

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:50 AM Oct 17 2024

KOCHA mkongwe nchini, Fred Minziro
Picha: Mtandao
KOCHA mkongwe nchini, Fred Minziro

KOCHA mkongwe nchini, Fred Minziro, ametangaza kubeba mikoba ya kuiongoza Pamba Jiji FC ya Mwanza ambayo imetangaza rasmi kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu, Goran Copunovic.

Mserbia huyo amehudumu katika kikosi cha Pamba Jiji kwa miezi miwili.

Mwenyekiti wa Pamba Jiji, Biko Khotecha, amesema Minziro, ambaye ni mmoja wa makocha wenye uzoefu na soka la Tanzania atasaidiwa na kocha wa vijana chini ya miaka 20 wa timu hiyo, Mathias Wandiba.

"Bodi ya Wakurugenzi ilikaa na uamuzi uliotolewa ni Kocha Mkuu wa Pamba Jiji sasa atakuwa ni bwana Minziro, nimeambiwa atakuwa ndiye mkuu wa benchi la ufundi, hii ndiyo habari rasmi.

Kwa maana hiyo mashabiki wetu waelewe klabu yao imeachana na Goran, kitu chochote kitakachotokea baada ya hapa tutafahamishana, lakini hii ndiyo habari sahihi na kesho (leo), Minziro ataanza kazi  kwenye Uwanja wa Nyamagana," alisema mwenyekiti huyo.

Goran, kocha wa zamani wa Simba na Tabora United, aliiongoza Pamba kwenye michezo saba ya Ligi Kuu bila kupata ushindi, ikitoa sare nne, kupoteza mitatu, ikiburuza mkia na pointi zake nne.