Wachezaji Simba wapewa angalizo usajili dirisha dogo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:37 AM Oct 08 2024
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu hiyo, Salim Abdallah 'Try Again',
Picha:Mtandao
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu hiyo, Salim Abdallah 'Try Again',

KLABU ya Simba imesema itafanya usajili wa wachezaji wapya kipindi cha dirisha dogo la usajili na kuondoa wale ambao watashindwa kuonesha ubora wao mpaka kufikia Desemba na Januari mwakani.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu hiyo, Salim Abdallah 'Try Again', amesema kuwa kwa sasa wana malengo makubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano ya ndani na nje ya nchi huku ikiwa imefanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi, hivyo wanategemea wachezaji waliopo kuonesha ubora na kuipambania klabu na si vinginevyo.

"Ni kweli, tutaboresha tena kikosi chetu kipindi cha dirisha dogo, tunaangalia wachezaji ambao wamefanya vizuri na wapo kwenye ubora na wapambanaji kuipigania nembo ya klabu tutabaki nao, wale ambao wameshindwa kuonesha ubora wao kwa namna moja ama nyingine au kwa sababu mbalimbali, tutawapunguza ili kuleta wengine ambao wanaweza kuleta upinzani katika kikosi chetu," alisema Try Again.

Mjumbe huyo ambaye ni Mwenyekiti wa zamani wa Bodi ya Wakurugenzi, alisema wanataka kuifanya Simba kuwa klabu tishio si Tanzania tu, bali Afrika nzima, hivyo watasaka mchezaji yeyote mzuri ambaye anafaa kuicheza klabu yao na kumleta kwenye kikosi chao.

"Jambo kubwa ni kuhakikisha Simba inarejea katika ubora wake, mimi nilipomwachia kijiti Mohamed Dewji, tulikubaliana kwamba lazima Simba irudi kwenye ubora wake na kwa mbali mmeanza kuona mabadiliko.

"Tumefanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chetu, tumesajili vijana wengi wadogo ambao wanahitaji muda kuweza kuendana na mazingira ya mpira wetu.

"Unaweza kuona wachezaji wengi tuliowaleta wa kikosi cha kwanza, pia tumesajili vijana wa ndani ili kujifunza kutoka kwa hawa tuliowaleta," alisema.

Baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu msimu uliopita, klabu hiyo iliondoa wachezaji wake wengi waliokuwa tegemeo kwenye kikosi hicho kwa muda mrefu, akiwamo nahodha, John Bocco, Clatous Chama, Saido Ntibazonkiza, Sadio Kanoute, Kennedy Juma na wengine wengi, huku ikisajili wachezaji 14 wa ndani na nje ya nchi ambao tayari wameiwezesha timu hiyo kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na tayari imeshacheza mechi tano za ligi, ikishinda nne na sare moja.